Na DERICK MILTON
WANANCHI wa Kijiji na Kata ya Ngulyati Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wamedai kuwapo mchezo mchafu kutoka kwa wahudumu wa Kituo cha Afya Ngulyati kuandika taarifa za wagonjwa hewa.
Madai ya hayo ya wananchi yalitolewa juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika mjini Ngulyati.
Wananchi hao walisema wahudumu hao wamekuwa wakifanya hivyo ili kutumia dawa kwa matumizi yao binafsi huku wazee wakinyimwa huduma za matibabu bure kama inayotakiwa.
Mmoja wa wananchi hao, Ramadhani Kuyege, alisema imekuwapo tabia ya wahudumu wa afya katika kituo hicho kuandika taarifa za wagonjwa hewa.
Alisema watumishi hao pia wamekuwa wakitumia dawa hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa, hali ambayo imesababisha kituo hicho kukosa dawa kwa muda mrefu.
“Huu mchezo ni mkubwa kwenye hiki kituo, wanaiba dawa wanapeleka kwenye maduka yao na nyingine wanawauzia wenye maduka ya dawa na sisi wananchi tunakosa tunabaki kuhangaika kila siku,” alisema Kuyege.
Minza Maduhu alidai kuwa kila mara kituo hicho cha afya kimekuwa kikosa dawa na wamekuwa wakiambulia dawa moja tu ya Panadol.
“Sisi wazee kila siku tunafukuzwa, tunaambiwa lazima tutoe fedha hakuna huduma za bure wakati kila siku viongozi wanatueleza wazee wanapata huduma bure.
“Kituo hiki hakina dawa kila siku wagonjwa wananunua dawa kwenye maduka ya dawa muhimu,” alisema Minza.
Kutokana na malalamiko hayo, RC alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji kumpelekea taarifa ya matumizi ya Sh milioni 10 ambazo zinatolewa na Wizara ya Afya kwenye kituo hicho.
“Kituo hiki kipata pesa kila mwaka Sh milioni 10 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya… niagize kufikia Jumatatu mkurugenzi afike ofisini kwangu kuniletea taarifa ya matumizi ya fedha hizo,” alisema Mtaka.