31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

WASOMI HAWATETEREKI KWA DHORUBA  – MUHONGO

 

Na SHOMARI BINDA


MBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka wananchi wa jimbo lake kuhakikisha wanawasomesha watoto wasiweze kuteteleka katika  maisha yao.

Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni mara ya kwanza kuzungumza na wananchi wa jimbo lake ikiwa ni miezi minne  tangu  alipojiuzulu  uwaziri wa Nishati na Madini  kwa kushindwa kusimamia suala la mchanga wa dhahabu unaosafirishwa nje kwenye makontena.

Alikuwa akizungumza baada ya kufunguliwa  nyumba za watumishi wa afya, tanuru la kuchomea taka na vyoo kwa ajili ya wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Murangi.

Mradi  huo  umefadhiliwa na ubalozi wa Japan.

Prof. Muhongo alisema elimu ndiyo mkombozi jamii kwa sababu  pia   wanaweza kupatikana  wataalamu wa afya.

Alisema wananchi wanapaswa kuzingatia   elimu kwa watoto  kuweza kuwapata wataalamu wa kada mbalimbali hasa wanasayansi ambao ni vigumu   kuteteleka kutokana na taaluma zao.

“Mtu aliyesoma hawezi kuteteleka hata ije dhoruba ya aina gani…nawaomba wananchi mlitilie mkazo suala la elimu tuweze kuwapata wataalamu wengi ambao katika siku za usoni waweze kutoa  huduma kwenye vituo vyetu na kuyatumia majengo haya,”alisema.

Prof.  Muhongo aliwataka wananchi kuacha kuitegemea serikali na wafadhili katika kufanikisha mambo yao ikiwamo ujenzi wa majengo ya zahanati na nyumba za wauguzi.

Aliwashauri  wajitoe katika kuchangia wenyewe kabla ya kuletewa misaada.

Alisema wananchi wanapaswa kujitoa na kuchangia kwa mali na nguvu zao katika ujenzi wa miradi mbambali yakiwamo majengo ya madarasa na maabara  kuweza kuzalisha wasomi wengi watakaoweza kusaidia taifa na jamii kwa ujumla.

Balozi wa Japan   nchini, Masaharu Yoshida, alimshukuru Profesa Muhongo  kwa kupendekeza mradi huo na kusaidia wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao umekamilika kwa viwango.

Alisema ubalozi wa Japan ulitoa  Sh milioni 150  kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya wafanyakazi, choo cha wagonjwa, tanuru la kuchomea taka   hospitalini   ambavyo vyote vimekamilika kwa viwango.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Flora Yongolo, alisema mradi huo umetekelezwa kwa ubora wa viwango vya serikali ya Tanzania.

Alisema mradi umelenga kupunguza adha ya makazi kwa watumishi wa Kituo cha Afya Murangi na uboreshaji utoaji  na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles