Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM
KUNDI la matapeli limeibuka katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoani Tanga.
Kundi hili linajitambulisha kama wawakilishi wa Kampuni ya ujenzi ya Alliance Contractors, limetangaza nafasi za kazi 7,000 kati ya 10,000 katika ujenzi huo wa bomba la gesi, huku Serikali ya Mkoa wa Tanga ikiwa haitambui suala hilo.
Baada ya kuonekana kwa tangazo hilo, gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela ili kupata ukweli wake, lakini naye alipigwa butwaa huku akiwatahadharisha Watanzania kutoingia katika mtego huo wa matapeli.
“Suala la ujenzi wa bomba huwa kuna utaratibu, hadi sasa hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa ili kujua nani atajenga nini na wapi, sasa hao wanaotoa matangazo ya ajira, tena kwa kutumia jina la Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ninapenda kuwahadharisha Watanzania waogopeni, hao ni matapeli tu.
“Ninapenda kuwaambia Watanzania wote kwamba kila hatua ambayo itafanyika katika mradi huu, mamlaka za Serikali zitaeleza kwa umma na hakuna kificho katika suala hili kwa sababu ni jambo lenye masilahi kwa taifa,” alisema Shigela.
Mmoja kati ya watu wanaodaiwa kuwa wawakilishi wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi Mkomesheni, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alidai wana nafasi za kazi 4,000 kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga.
Alipopigiwa tena simu kwa mara ya pili ili kuulizwa kama tangazo hilo la ajira linatambulika na mamlaka za Serikali, alikata simu na hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.