Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
UBALOZI wa Kuwait Nchini umehaidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya kwa kuhakikisha inaleta wataalamu wa kutosha nchini.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Balozi wa Kuwait nchini, Jaseem Al Najem alipokuwa akizindua visima vya maji katika Shule ya Msingi, Magoza iliyoko Tabata Kisukuru Jijini Dar es Salaam.
Alisema mkakati wa nchi hiyo ni kuhakikisha kuwa shule za msingi nchini zinakuwa na huduma ya maji pamoja na miundombinu bora ili kuwafanya wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.
“Mkakati wetu ni kuzisaidia shule ziweze kuzalisha wataalamu wa kutosha kwenye maeneo mbalimbali hivyo tunaamini kuwa kupitia upatikanaji wa huduma muhimu mashuleni ikiwamo maji, uzio, kompyuta na hata michezo ni mambo ambayo yatasaidia kuwaweka wanafunzi kwenye hali nzuri.
“Hivyo kwetu sisi tunakauli mbiu ya ‘kisima kila shule’ hivyo tunatarajia kuzifikia shule nnyingi zaidi nchini zinazokabiliwa na uhaba wa maji ili kuwafanya wanafunzi wapate muda wa kujisomea kuliko kuutumia kutafuta maji,” alisema Jaseem Al Najem.
Aliongeza kuwa kisima hicho kimegharimu dola 9,000 sawa na Sh milioni 20, gharama ambazo alisema kuwa zimeongezeka kutokana na eneo hilo kuwa na miamba mikubwa.
Upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Human Relief Foundation, ambao ndio wanaohusiska na kusimamia uchimbaji wa visima hivyo kwenye shule mbalimbali hapa nchini, Mbarak Baghumesh alisema kuwa kisima hicho kwenye shule hiyo kilikuwa ni cha 41 na kwamba lengo ni kufikisha visima 100 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Adhma yetu ni kufikisha visima 100 kabla ya mwaka huu kuisha ili kuwasaidia watoto wa kitanzania na wananchi wanaozunguka shule husika kuweza kupata huduma ya maji ambayo ni tatizo kubwa kwa shule nyingi nchini.
“Hivyo kikubwa ni kuhakikisha kuwa walimu na wanafunzi kuhakikisha kuwa wanavitunza visima hivi kwaajili ya manufaa yao na kuvifanya vidumu zaidi,” alisema Baghumesh.
Akipokea msaada huo Diwani wa Kata ya Kisukuru, Joseph Saenda (CCM), alisema msaada huo utaondoa adha ya maji ambayo imedumu kwenye kata yake hiyo kwa kipindi kirefu ikiwamo pia kuwafanya wanafunzi kushindwa kusoma vizuri.
“Kwaniaba ya wanachi wa Kisukuru tunatoa shukrani za dhati kwa Ubalozi wa Kuwait na kwa taasisi ya Human Relief Foundation kw akutukabidhi kisima hiki na si tunahaidi kukitunza ili kiendee kuwa msada kwetu,” alisema Saenda.
Naye Mwalim Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magoza, Kahwa Ebikuru, alisema kuwa kupata msaad huo wa maji kutawafanya wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea na hivyo kuongeza ufaulu wao.