Na MWANDISHI WETU
SIKU mbili baada ya kuanza kusambaa mitandaoni na kuchezwa kwenye vituo mbalimbali vya redio, wimbo wa Msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’, umeibua maswali mengi.
Maswali yanaanzia kwenye jina la wimbo huo aliouita ‘Zimbabwe’, ambapo kwenye mashairi yake anasema ‘nakwenda Zimbabwe’, ambapo wengi wamejiuliza kwanini wimbo wa kuelezea kutekwa kwake aupe jina kama hilo.
Kwenye utambulisho wa wimbo huo katika moja ya kituo cha redio, msaani huyo aliwakilishwa na mkewe, Nancy Mshana, ambaye alisema mumewe ameshindwa kufika kwa sababu amesafiri kwenda Zimbabwe.
Mashairi mengine yaliyo kwenye wimbo huo ambayo yanaibua maswali ni pamoja na pale anaposema ‘na ripoti ya upelelezi vipi akiteka mtekaji?”
Anasema hayo wakati ambapo mpaka sasa, haijajulikana ni nani aliyemteka.
Katika wimbo huo aliouachia wiki hii sanjari na video yake, Roma ameeleza zaidi kuhusu maisha yake na namna alivyotekwa na watu wasiojulikana miezi michache iliyopita.
Huu ni wimbo wa kwanza kwa msaani huyo tangu kuibuka kwa taarifa za kutekwa kwake Aprili mwaka huu, na baadae kuonekana tana akiwa kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay.
NANI ALIYEMTEKA?
Katika wimbo wake huo, alianza kuimba kwa kusema, “Wengi mlijiuliza aliyeniteka ni maaskari, mkanitafuta vituo vyote, Central hadi Sitakishari, wakasema hawajui nilipo.
“… mama alikwenda hadi mochwari… dah! Ya Kaisari, mwachie Kaisari. Machozi yenu yatalipwa mimi nafunga na kusali.”
Wimbo huo unaeleza pia, namna ndugu, mashabiki na jamii kwa ujumla walivyoguswa na kutekwa kwake na kwamba watalipwa na Mungu.
MATESO
Anasema angeweza kuwa tayari hata kufa kwa sababu ya harakati lakini kilichokuwa kikimuumiza zaidi ni familia yake.
“Mwanangu alimuuliza mama, baba lini atarudi? Na mke wangu aliwaliza, kuwashukuru sina budi… mimi siyo tu rapa ni baba wa familia na watoto nawapa mahitaji kama isemavyo Biblia…
“Kipi bora? Nife mseme nilikufa kiharakati, siogopi kufa ila nawaachaje wanaobaki? Je, nani kati yenu mwanangu atampa malezi, wapi atapata mahitaji, wapi atapata mapenzi?
“Nilipokuwepo sikuwa najua hii saa nne, hii saa nane… nilichohitaji nitoke mzima na ndugu zangu tuonane. Nimechapwa mijeledi, nimevunjwa bila huruma, asante mliopaza sauti, nimeiona nguvu ya umma.
“Siku tatu nimefungwa macho, mikono imefungwa nyuma… nakwenda Zimbabwe… yelele mamaaaaa.”
Aidha alitoa ufafanuzi kuhusu namna alivyotekwa ambapo alisema, ingawa inaelezwa kuwa alitekwa na watu waliomwingiza kwenye gari aina ya Toyota Noah, habari hizo si sahihi.
Alilaumu kitendo chake cha kutekwa akikiita kuwa ni cha uhuni wa kishamba huku akihoji waliomteka walikwenda wenyewe au kwa walitumwa.
Akizidi kuibua maswali katika wimbo huo, Roma alisema waliotabiri ataonekana kabla ya Jumapili, anawashukuru kwa vile utabiri wao ulitimia.
Roma alitekwa Aprili mwaka huu na kuzua maswali yaliyokosa majibu kuhusu nani aliyemteka na wapi alipokuwa.
Roma alitekwa akiwa na wenzake, Monii Central Zone, Bin Laden na Imma, ambaye ni mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio za Tongwe Records iliyopo Masaki, Dar es Salaam, J Murder.
Ilidaiwa kuwa walivamiwa wakiwa studioni hapo majira ya saa 1:30 na kutekwa na watu wasiojulikana.