28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

POLISI DAR YAKAMATA WEZI SUGU

 

 

MARGRETH MWANGAMBAKU na ABDALLAH NG’ANZI (TUDARCO)

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa sugu 10 wa uporaji mali za raia kwa njia ya pikipiki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Kamisha Msaidizi wa Polisi (DCP) Lucas Mkondya, alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni ya kudhibiti uhalifu inayoendelea.

Kamanda Mkondya aliwataja kwa majina viongozi wa genge hilo la uhalifu kuwa ni Carlos Thobias (18), Boniface George (20), Akida Twaha (21) na Deogratius Lyamuya (26), wote wakiwa wakazi wa Kimara.

“Tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 10 wanaojihusisha na uhalifu katika maeneo mbalimbali na kuwataja wenzao wengine 13 ambao wanajihusisha na uporaji kwa njia ya pikipiki,” alisema Mkondya.

Alisema watuhumiwa wote walikiri kuhusika pamoja na kushiriki matukio ya kupora mali za wananchi, zikiwamo simu, televisheni na laptop.

“Watuhumiwa hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Kimara, Sinza, Magomeni, Kawe na katikati ya Jiji, tumewakuta na televisheni moja, laptop moja na simu 9 za aina tofauti,” alisema Kamanda Mkondya.

Aidha, alisema ndani ya kipindi cha wiki moja Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata jumla ya watuhumiwa 275 kwa makosa mbalimbali ya kukutwa na dawa za kulevya pamoja na uhalifu.

“Operesheni hii ni endelevu, jumla ya kete 96 za dawa za kulevya tumezikamata, puli 156, misokoto ya bangi 86, magunia 15 ya bangi pamoja na pombe haramu aina ya gongo lita 60,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mkondya alisema kuwa, jeshi hilo litaanza operesheni maalumu ya kudhibiti wapiga debe katika vituo mbalimbali vya daladala kuanzia Agosti 14, mwaka huu.

“Kuanzia Jumatatu hatutaki wapiga debe katika vituo vyote vya mabasi, kwa sababu wahalifu wengine hutumia fursa hiyo kufanya uhalifu, hasa nyakati za usiku, nasisitiza ni marufuku kuwapo kwa wapiga debe katika kituo chochote cha daladala,” aliongeza Mkondya.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimefanikiwa kukusanya jumla ya Sh milioni 463 ndani ya kipindi cha wiki moja, ikiwa ni tozo za makosa mbalimbali ya usalama barabarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles