Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
TIMU ya Singida United, imeendelea kujiimarisha baada ya kumchukua kwa mkopo mshambuliaji wa kati kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Michelle Katsvairo kwa ajili ya kuitumia katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ujio wa Katsvairo atakayeitumikia kwa mwaka mmoja umekamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni, ambapo wengine ni Elisha Muroiwa, Tafadwaza Kutinyu na Simbarashe Nhivi wote kutoka Zimbabwe pamoja na Shafik Batambuza wa Uganda na Danny Usengimana kutoka Rwanda na Michael Rusheshangoga.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Patrick Sanga, alisema wamemchukua mchezaji huyo kwa mkopo wa mwaka mmoja akitoke Kaizer Chief.
“Katsvairo anakuwa ni mchezaji wa saba wa kigeni baada ya kuachana na Wisdom Mtasa, aliyetimkia Stand United, hivyo tunaamini ataisaidia timu yetu na kutuletea matokeo mazuri,” alisema.
Alisema mchezaji huyo aliwasili jana hivyo ataenda kuungana na wachezaji wenzake moja kwa moja na kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.