27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAOMBWA KUTUPA OMBI LA WABUNGE CUF

NA KULWA MZEE

DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeombwa kutupilia mbali maombi yaliyofunguliwa na wabunge wanane na madiwani wawili wa Chama cha Wananchi (CUF), wakitaka wabunge wateule wa chama hicho wasiapishwe kwa sababu haina mamlaka ya kutoa uamuzi kwa amri wanazoziomba.

Hoja hizo ziliwasilishwa jana na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabrieli Malata mbele ya Jaji Lugano Mandambo, baada ya wadai kuwasilisha maombi.

Wadai katika maombi hayo, ni Mbunge Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahali Ngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na

Halima Ali Mohamed na madiwani ni Elizabeth Sakala na Layla Madiba.

Wadaiwa ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Katibu wa Bunge, Bodi ya Wadhamini CUFna wabunge wateule wote.

Akipinga maombi yao, Malata alidai njia waliyotumia kufikisha mahakamani maombi hayo si sahihi, kwani kifungu hicho cha Sheria ya Jala kinatoa ridhaa ya kutumia sheria za Uingereza na ukishapata ridhaa hiyo unapaswa kueleza unatumia sheria ipi.

Alidai kufikisha maombi hayo mahakamani ni kuisumbua mahakama, wanatafuta nafuu ya jambo moja katika mamlaka mbili tofauti kwani wakati wanaomba zuio na wamewasilisha rufaa katika mkutano mkuu wa chama hicho.

“Mheshimiwa Jaji, mahakama hii haina mamlaka ya kutoa amri wanazoomba kwa sababu mhimili wa Bunge unatekeleza majukumu yake kikatiba, kuna mazingira ambayo mahakama inaweza kutoa amri kwa muhimili mwingine lakini si mazingira kama haya,”alidai Malata.

Wakili anayewakilisha Bodi ya Wadhamini CUF na wabunge wateule, Mashaka  Ngole alidai maombi hayo ni batili kwa sababu  yamewajumuisha wabunge wateule kuwa ni wadaiwa, wakati katika kesi ya msingi hawapo  hivyo aliomba yatupwe.

Akijibu,Wakili Peter Kibatala alidai kifungu cha sheria alichotumia ni sahihi pingamizi lililowasilishwa halikidhi vigezo vya kuwa pingamizi.

Alidai amri ya zuio inaweza kutolewa na mahakama hata bila kuwapo kesi ya msingi, hivyo hoja ya wabunge wateule kutokuwepo katika kesi ya msingi haina mashiko.

Kibatala aliomba mahakama hiyo, itoe amri ya kwamba hali iliyopo iendelee kuwa hivyo mpaka kesi zilizopo mahakamani zitakapotolewa uamuzi.

Jaji Mwandambo, alisema hawezi kutoa amri yoyote kwa sasa, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pingamizi na aliruhusu Wakili Kibatala kufanya marekebisho ya hati ya madai katika kesi ya msingi ambayo itatajwa Agosti 21 mwaka huu.

Katika maombi hayo, wabunge waliovuliwa uanachama na ubunge wanaomba mahakama itoe amri ya kuzuia wabunge wateule kuapishwa hadi kesi ya msingi itakapomalizika na amri ya kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles