24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MKOJO WA MASOGANGE WAKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA

NA KULWA MZEE

DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeelezwa kuwa  mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange, ulibainika kuwa na dawa za kulevya aina ya Heroine, baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Hayo yalidaiwa jana na Mkemia Elias Mulima kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kutumia dawa za kulevya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri.

Wakili wa Serikali, Constatine Kakula  akimwongoza Mulima, alidai Masogange alipelekwa  ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam, Februari 15, mwaka huu na askari wawili kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Koplo Sospether na WP Judith.

Alidai askari hao, walitaka mshtakiwa afanyiwe kipimo kuthibitisha kama anatumia dawa za kulevya.

Mulima alidai alifanya usajili na kuipa sampuli hiyo namba ya maabara 446/2017 na kwamba  WP Judith alikabidhiwa kontena maalumu ili mshtakiwa akaweke sampuli ya mkojo.

Alidai baada ya kupokea sampuli ya mkojo wa mshtakiwa, alifanyia uchunguzi kupitia kemikali ambazo zinachunguza dawa za kulevya kwenye mkojo na kupima kwa kutumia mtambo.

Alidai baada ya uchunguzi ilibainika kuwa mkojo wake una chembechembe za dawa za kulevya aina ya Heroine ambazo ni Diacety Imophine na uchunguzi ulibaini mkojo huo una chembechembe za dawa za kulevya aina ya Oxazepam.

Shahidi huyo, alidai aliandaa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sampuli hiyo ya mkojo ambapo alitia saini na kuthibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mkemia Mulima, alimtambua mshtakiwa Masogange mahakamani hapo  ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo.

Pia alidai anaweza kuitambua taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na saini yake, muhuri wa moto wa maabara ya  mkemia mkuu  wa serikali. Shahidi aliitambua taarifa hiyo baada ya kuoneshwa na Wakili wa Serikali na kuiomba mahakama kuipokea kama kielelezo kwenye kesi hiyo.

Ombi hilo, lilipingwa na mawakili wa Masogange, Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza kwa madai haijakidhi vigezo vya sheria.

Nkoko, alidai utaratibu wa kisheria haukufatwa kwani  kabla ya mtuhumiwa aliyeko chini ya ulinzi wa polisi kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, ofisa wa polisi alitakiwa kuwasilisha maombi mahakamani ndipo amri itolewe.

Alidai katika ushahidi wake, mkemia huyo hajaeleza kama ofisa wa polisi alipeleka amri ya mahakama kutoka mahakama yoyote ile.

Alidai ripoti ipo kinyume na sheria, mahakama ina njia moja tu ya kuikataa na sio kuikubali. Sheria ipo wazi hivyo aliomba mahakama ikubali pingamizi ispokewe taarifa hiyo.

Naye Wakili Simwanza, alidai ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya ombi la Jeshi la Polisi kwenda kwa mkemia mkuu kwa ajili ya kufanya vipimo.

Alidai ripoti hiyo ipo yenyewe bila ya kuambatanishwa na hiyo fomu, hivyo haiwezi kupokelewa na kutumika kama kielelezo.

Wakili Kakula akijibu hoja hizo alidai mapingamizi hayo hayana mashiko wala miguu ya kusimamia.

Alidai fomu ambayo haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu viwili tofauti na hata uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.

Alidai taarifa ya mkemia inawasilishwa na mkemia na ile ya polisi inawasilishwa na polisi.

Kuhusu hoja ya sampuli ya mkojo, Kakula alidai kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kimeweka mazingira ambayo ofisa wa polisi atawasilisha maombi mahakamani kuweza kuchukua sampuli.

Alidai iwapo mtuhumiwa anakataa kuchukuliwa sampuli ya mkojo, hivyo atawasilisha ombi mahakamani ili iweze kutolewa amri.

Kakula alidai katika pingamizi lao upande wa utetezi haijaeleza kwamba mshitakiwa alikataa kupima, akalazimishwa. Aliomba mapingamizi hayo yatupiliwe mbali.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo  hadi Agosti 28, mwaka huu  kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa ama kupokelewa kwa taarifa hiyo ama la.

Masogange anadaiwa kati ya Februari 7 na 14, mwaka huu maeneo yasiyojulikana ndani ya  Dar es Salaam  alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Anadaiwa kuwa kati ya tarehe hizo alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles