Na Mwandishi Wetu,
KATIKA mabadiliko ya sheria yaliyofanyika hivi karibuni na Bunge la Tanzania ni sheria ile inayozuia kampuni za madini kutoweka fedha zake nje ya nchi na badala yake fedha hizo zije nchini na zitatoka kama gawiwo baada ya kufanya hesabu husika na kila upande kupata chake.
Ingawa ni ngumu kumeza, makampuni hayo hayana la kufanya katika muundo mpya wa Sheria Tanzania kwani hii inatokana na ukweli kuwa katika mabadiliko hayo maliasili imebainishwa wazi kuwa ni mali ya taifa na kwa Watanzania wote.
Hivyo basi ni marufuku kwa kampuni za madini kuweka fedha nje kwani Serikali inatakiwa iwe na hisa zisizopungua asilimia 16.
“Sasa kampuni za madini zinazofanya kazi zake nchini hazitaruhusiwa kuhifadhi fedha nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia mashauri ya mikataba hiyo yatafanyika ndani ya nchi na si katika mahakama na mabaraza ya nje, Bunge limepitisha Sheria katika kulinda rasilimali za nchi, ‘ Sheria za Mabadiliko ya Sheria 2017 ( yaani Written Laws Miscellaneous Act, 2017 Natural Wealth and Resources, Permanent Sovereignty) Act 2017 na Natural Wealth and Contracts Review and Renegotiation of Unconscionable Terms Act 2017) zinadai.
Sheria hizo wanadai wengi ni sawa na tangazo la vita, mtazamo ambao Rais Magufuli ameuona na Waziri wake wa Katiba na Sheria Profesa Palamaganga Kabudi kuukubali
Aidha, Bunge limepewa nguvu ya kupitia makubaliano ya mikataba ya maliasili na rasilimali za nchi.
Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017, Profesa Kabudi alisema sheria inaeleza mapato yote yanayotokana na rasilimali na maliasili na utafutaji, uchimbaji au umiliki na utumiaji wa rasilimali za Taifa, yanahifadhiwa katika taasisi za kifedha za ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
“Itakuwa ni kosa kuweka fedha hizo nje ya nchi isipokuwa gawiwo ambalo mwekezaji ataruhusiwa kutoa nje ya nchi kwa mujibu wa sheria za nchi za Tanzania,” alieleza Profesa Kabudi na kuongeza kuwa pia sheria inatamka kuwa mashauri kuhusu maliasili na rasilimali za nchi chini ya mamlaka ya nchi hayatafanyika chini ya mahakama na mabaraza ya nje.
Sheria hiyo imekubalika kutumika pande zote mbili za Muungano, bila kuathiri mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya usimamizi wa rasilimali za nchi.
Sheria pia inazuia usafirishaji wa maliasili bila kuongeza thamani, lengo ni kuleta maendeleo na kutekeleza azma ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda.
Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017, kutokana na maelezo ya Profesa Kabudi, alisema inawezesha wananchi kupitia Bunge, kupitia mikataba inayohusu rasilimali na maliasili ya nchi ambayo imefungana na Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kujiridhisha kama masharti, makubaliano na mikataba haina masharti hasi na yanakinzana na masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla na kuishauri Serikali.
“Sheria imeipa nguvu bunge kupitia mikataba yote inayohusiana na malisili za nchi na rasilimali zake iliyoingiwa na Jamhuri ya Muungano ili kujiridhisha masharti yaliyomo kwenye mikataba hiyo yamezingatia masilahi ya Watanzania. Na endapo mikataba haitii masilahi ya Watanzania, basi Bunge liweze kuishauri Serikali kufanya majadiliano na wahusika wengine katika mikataba kwa lengo la kuondoa masharti hasi yasiyokuwa na manufaa kwa Taifa,” alifafanua.
Nchi yaonesha ubabe
Prof. Kabudi aliongeza: “Endapo Serikali haitafikia makubaliano yenye tija kwa wananchi na taifa ndani ya muda utakaokubaliwa na pande zote basi masharti yote hasi yatachukuliwa kwamba yamefutwa na si sehemu ya mikataba na Serikali haitakuwa na wajibu wowote wa kutekeleza masharti ambayo yamebainika kuwa hasi.” Imekubalika kuwa Serikali itapitia mikataba yote ya madini ya sasa kwa kuzingatia sheria mpya zilizopitishwa na Bunge.
“Miswada hii inalenga kuleta mapinduzi makubwa katika kulinda rasilimali na maliasili ya nchi, dhana ya miswada hii ni ukombozi wetu na mapinduzi ya Watanzania wote,” alieleza Profesa Kabudi.
Alinukuu insha ya falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema: “Mapinduzi haya yanayotakiwa ni kwa wote na si kwa wachache, tulipoonewa tulionewa wote, tuliponyonywa tulinyonywa wote, tulipopuuzwa tulipuuzwa wote, ni unyonge wetu sote kwa pamoja ndio uliotufanya tukaonewa, tukanyonywa na kupuuzwa, mapinduzi tunayoyafanya sasa, ni lazima yawe yetu kwa pamoja ili Mtanzania asiwe mnyonge na unyonge wake ukatumiwa kumnyonya na kupuuza.”
Miswada mitatu ya mabadiliko ya Sheria na wabunge ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017 na ule wa sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi wa mwaka 2017.
Maoni ya Kamati
Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja, Dotto Biteko, akitoa maoni aliitaka Serikali kuboresha zaidi mifumo na uwezo wa mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki nchini ili vishughulikie mashauri yanayojitokeza na yatakayoweza kujitokeza kutokana na masharti ya uwekezaji yaliyomo katika miswada hiyo.
Alisema pia Serikali ianze haraka mchakato wa ujenzi wa mitambo ya kuchakata au kuchenjua malighafi za rasilimali nchini ili kuwezesha wavunaji wa rasilimali hizo kupata huduma hiyo nchini.
Aidha, alisema Serikali iimarishe mfumo wa utendaji wa benki na taasisi za kifedha ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia taasisi mbalimbali na kampuni kubwa za uwekezaji nchini.
Biteko aliishauri Serikali kuhakikisha utungaji wa kanuni unafanyika mapema ili kuwezesha utekelezaji bora na wa haraka wa sheria iliyotungwa.
Upinzani wataka mali isiwe chini ya Rais
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepinga kitendo cha Serikali au Bunge kutumia kifungu cha 5 (2) cha sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili wa mwaka 2017 ambacho kimeweka umiliki wa rasilimali na maliasili za nchi mikononi mwa Rais kwa niaba ya wananchi wa Tanzania. Lakini ardhi yote iko chini yake.
Kambi rasmi bungeni imesema kuwa kifungu hicho ni hatari kwani kinaweza kuleta madhara makubwa kwa Taifa kisipoangaliwa kwa uzalendo uliotukuka kwani endapo anaweza kupatikana rais ambaye si mzalendo nchi inaweza kutumbukia pabaya.
“Mikataba hii imezipa kinga kubwa sana kampuni za madini ambazo zimesaini mikataba na Serikali ikiwa ni pamoja na kuzuia kutumika kwa sheria mpya ambazo zinapitishwa na Bunge kwa kampuni hizo kuanzia mikataba hiyo inaposainiwa,” yalikuwa maoni ya upinzani yaliyosomwa na Mbunge Cecilia Paresso.
Naye John Heche, akiwasilisha maoni ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba inayohusu maliasili za nchi wa mwaka 2017, alieleza kuwa upinzani umekuwa ukikemea suala la kupeleka bungeni miswada ya sheria bungeni kwa hati ya dharura. Ana hofu hazitajadiliwa kikamilifu na hivyo kukosa umuhimu kwa taifa.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alitoa mwanga kuhusu hilo na alisema Bunge linapotunga sheria ni wakati muhimu wa kuwa makini na kwamba miswada hiyo ilihitaji muda wa kutosha.
Alisema anataka kuamini kuwa Rais aliyepo ni mzalendo na anapenda watu. “Najiuliza kwa mamlaka aliyopewa Rais siku akija mtu si mzalendo kama Magufuli nataka kuamini hivyo akatokea hata upande huu hata Chadema kwa sababu huku hakuna malaika au akitokea CUF nako hakuna malaika, akatokea rais si mwaminifu na amepewa mamlaka kubwa ya kusimamia rasilimali basi atauza Taifa hili,” alieleza Lema.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema: “Sheria hizi mbili ni za kimapinduzi na kwamba chochote kilichopo juu na chini kwenye nchi yetu ni mali yetu, lakini mfumo wa uzalishaji ni ule ule, sheria iliyopita ina umiliki, sheria ya mwaka 1979 ilikuwa na umiliki, si jambo jipya lakini tubadilishe mfumo wa uwekezaji.”
Alipendekeza kuwa badala ya kuwapa uwekezaji, Serikali imiliki rasilimali hizo na kutoa ukandarasi kwa kampuni kutoka nje ili wakichimba faida igawanywe kulingana na makubaliano. Huu ndio ukweli wa mambo na inatakiwa iwe hivyo.