27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI BOMBA MAFUTA KUWEKWA JIWE MSINGI TANGA

Na Mwandishi Wetu,

HISTORIA iko mbioni kutengenezwa katika Mkoa wa Tanga ambapo bandari ya Tanga itakuwa kitovu cha mradi mkubwa wa usafirishaji  wa mafuta ghafi na itawekwa jiwe la msingi.

Bomba hilo linalojulikana kama East African Crude Oil Pipeline (EAPCO), lilianza mwaka 2015 marais wa nchi ya Tanzania na Uganda walipoweka saini ya nchi zao na zitajenga bomba hilo baada ya Tanzania kuishinda Kenya katika zabuni ya kujenga bomba hilo nchini mwake baada ya ushindani mkubwa.

Awali Serikali ya Uganda ilitaka bomba hilo lipite Kenya lakini Tanzania ilipoonesha nia ya ujenzi ikaonekana ina mema zaidi kuliko Kenya na hivyo kuruhusiwa kutoa maelezo ya kufanikisha mradi.

Akizungumza kwenye kipindi cha Clouds 360, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapulya Musomba, amesema Agosti 5, marais Yoweri Museveni wa Uganda na Dk. John Magufuli wa Tanzania, wataweka jiwe la msingi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda pale mjini Tanga.

Itakuwa ni kitendo cha mwanzo na kina umuhimu wa kipekee cha kuashiria ujenzi wa bomba la umbali wa kilomita 1,430 ambalo asilimia 80 litakuwa katika ardhi ya Tanzania na linakisiwa kuwa litagharimu zaidi ya dola bilioni 3.5 katika ujenzi na hivyo kuleta faida kubwa katika uchumi wa nchi mbili hizi na kigezo cha wazi cha utengamano wa  uhakika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ratiba ya mradi inaonesha kutakuwa na hatua kuu tano za mradi ikiwamo kuweka saini za Serikali mbili, kusanifu mradi wa mkuza (FEED), ujenzi au utekelezaji wa mradi (Project Execution and Implementation), uteuzi wa mhandisi mwelekezi (Consulting Engineer), mtengenezaji mabomba ya ujenzi na mjenzi wa mradi maamuzi yalikwisha fanywa Aprili mwaka huu.

Mradi unategemea kuchukua kati ya miezi 24 hadi 30 kuanzia kuwekwa jiwe la msingi na hivyo hatua hiyo ni muhimu kwani inaashiria mwenendo wa mradi huo na uko kwenye hesabu ya utekelezaji mradi.

Wahusika na faida za mradi

Musomba anasema wahusika wakuu wa mradi ni Serikali mbili za Uganda na Tanzania na wengine Kampuni ya Mafuta ya Total ya Ufaransa (Total Oil SA), Kampuni ya Sino Pec ya Uchina na Tullow  Oil ya Uingereza/Ireland ambao kila mmoja majukumu yake ya mradi  yameainishwa vilivyo.

“Matanki makubwa ya mafuta ghafi yatajengwa Tanga  na Serikali inafikiria uwezekano wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta hayo mjini Tanga baada ya utafiti husika kukamilika ili kuongeza thamani na nchi kufaidika na uwepo wa mafuta hayo ambayo yamekisiwa kuwa ni hazina ya mapipa ya kiasi cha bilioni 1.7 ambayo yamethibitishwa na wadau wengine wa mafuta kama mtu wa tatu huria katika mradi,” alisema Musomba.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema faida za mradi huo ni nyingi ikiwamo ajira, ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, biashara na sekta ya usafirishaji.

Alisema Tanga kwa sasa ina bandari ambayo haijaendelezwa itaboreshwa zaidi wakati reli itabeba mzigo wa mabomba hayo pamoja na malori ya aina mbalimbali kupeleka mabomba kwenye vituo mbalimbali kwani kinachojengwa ni korido ya maendeleo na hivyo kufungua maeneo mbalimbali kwa uwekezaji na biashara kabla na baada ya ujenzi wa bomba hilo ambalo linakadiriwa kuwa litaajiri wafanyakazi 10,000 wakati wa ujenzi wa mradi na ni wa muda wa miaka miwili na nusu na 1,000 hadi 1,500 ni wa kudumu na asilimia 80  yao watatoka Tanzania kwani ndiyo yenye urefu mkubwa wa mradi na kubeba majukumu  makubwa na mengi.

“Kimkakati itathibitisha kuwa Tanzania ni salama kuwekeza  kwa wawekezaji toka nje yaani (FDI), kuthibitisha vile vile uthubutu na dhamira nzuri ya marais hao na hivyo Tanga iwe imara na tayari kwa ugeni huo mkubwa na muhimu,” alisema  Musomba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles