27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

WAJUMBE TIMU YA MAKINIKIA TANZANIA WANAPOTOKA

Mwandishi wetu

WAKATI Barrick Gold Corporation ikituma nchini wajumbe 13 kufanya majadiliano juu ya katazo la kusafirisha nje ya nchi mchanga wa dhahabu (makinikia), imeelezwa kuwa wajumbe wanaoiwakilisha Tanzania kwenye vikao hivyo wanatoka maeneo takriban 10.

Taarifa   iliyotolewa na Ikulu juzi, ilisema timu ya Tanzania inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi huku ile ya Barrick ikiongozwa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni hiyo, Richard Williams.

Profesa Kabudi kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea na mkufumzi wa sheria huku Williams  akiwa ni msomi wa masomo ya ulinzi na usalama   na mambo ya uchumi na biashara.

Mbali na viongozi hao wa timu hizo, majina ya wajumbe wengine kutoka kwenye timu ya Barrick hayajawekwa wazi licha ya picha zilizosambazwa na Ikulu jana kuwaonyesha wako 13, huku wale wa Tanzania wakiwa hawajaonyeshwa.

Wanapotoka wajumbe wa Tanzania

Juzi, MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, kutaka kujua majina ya wajumbe wengine wa Tanzania watakaoshiriki mazungumzo hayo, ambaye alisema:

“Watanzania wasiwe na hofu na tunaomba waiamini Serikali katika hili chini ya Profesa Kabudi, hakuna kitakachoharibika na hata wanaotaka wajumbe wa kamati hiyo wawafahamu wavute subira na wajenge imani kuwa Serikali yao”.

Hata hivyo gazeti hili katika uchunguzi wake, limebaini kuwa wajumbe hao watatoka   maeneo 10 nyeti.

Baadhi ya maeneo hayo ni   kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza usafirishaji wa mchanga huo ambazo matokeo yake ndiyo yaliyosababisha kupigwa marufuku  usafirishaji wa mchanga huo.

Kamati ya kwanza iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, ambayo ilipewa hadidu za rejea zilizojikita kujua kiwango cha madini kilichokuwa kwenye makinikia kwenye kontena 277 zilizopo Bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu na migodini.

Kamati ilibaini kiasi cha madini   kwenye mchanga huo ni kikubwa maradufu ikilinganishwa na kile kilichotajwa na migodi.

Kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osoro, ilijikita kuangalia masuala ya  uchumi na  sheria, ambayo nayo ilibaini kuwa nchi imepoteza matrilioni ya fedha.

Kutokana na umuhimu wa ripoti za kamati hizo, uwakilishi wao unatajwa kuwa muhimu kwenye kamati hiyo inayokutanisha maofisa wa Barrick ambao kupitia kampuni tanzu yao ya Acacia, walisema hajazipata ripoti za kamati za Rais.

Wajumbe wengine wanaotajwa kuwa kwenye kamati hiyo ni kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao kamati ya Profesa Osora ilitumia takwimu zake katika kujua kiasi cha mchanga uliosafirishwa nje ya nchi   tangu biashara hiyo ianze nchini.

Umuhimu mwingine wa wawakilishi wa TRA kwenye mkutano huo ni deni la Sh trilioni 424, fedha ambazo mamlaka hiyo hivi karibuni ilizipeleka kwa kampuni za Bulyanhulu Gold Mine Limited (“BGML”) Pangea Minerals Limited (“PML”), ambazo ndizo zinazimamia migodi ya Barrick na Acacia   nchini.

Pia wajumbe kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanatajwa kuwapo kwenye kamati hiyo kwa kuwa kiini cha majadiliano yote haya ni uchumi wa nchi ambao mmoja wa wasimamizi wake wakubwa ni benki hiyo.

Pia kamati ya Profesa Osora ilizungumzia umuhimu wa kuwa hifadhi ya madini ya dhahabu chini ya BoT,  kuimarisha shilingi na uchumi wa nchi.

Ili utekelezaji wa azimio hilo la kamati lifanikiwe, wajumbe wa BoT wanatajwa kuwamo kwenye mazungumzo hayo.

,Mbali na  Profesa Kabudi, wataalamu wengine wa sheria kutoka wizara yake   wanaelezwa kuwa ni kiungo muhimu kwenye mazungumzo hayo.

Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wataalamu wengine kutoka   ofisi yake wanaelezwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa, yanatarajiwa kuzungumzia suala la mikataba ya madini na sheria za nchini juu ya maliasili hiyo.

Wizara ya Nishati na Madini, mbali na kuwakilishwa na viongozi wake wakuu, ambao ni Waziri na Katibu Mkuu, inatajwa pia kutoa wawakilishi wengi kwa kuwa yenyewe ndiyo hasa inahusika kusimamia sekta hiyo.

Mbali na wajumbe hao watakaoingia kwa sababu ya ofisi zao, wajumbe kutoka sekta binafsi nchini wanatajwa kuhudhuria mazungumzo hayo.

Licha ya wasomi wanaoingia kwenye kamati hiyo kutokana na ofisi zao, inaelezwa kuna uwezekano pia wa kujumuishwa   wasomi wengine wa mambo ya uchumi na sheria.

Pia wajumbe kutoka nje ya nchi wanatajwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo hayo, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu kwa kuwa sasa itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya madini.

Kitakachojadiliwa

Ingawa sehemu kubwa ya mazungumzo hayo yanatarajiwa yatakuwa kuhusu ripoti mbili za kamati za Rais ambazo ndizo chimbuko la katazo la kusafirisha nje makinikia   na kuzaa mazungumzo yao, pia suala la mrabaha linategemewa kujadiliwa.

Suala jingine ni kodi ya Sh trilioni 424   na uhalali wa kusafirisha tena mchanga huo au uchenjuliwe nchini.

Wadau

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa akizungumza na gazeti hili, alisema serikali haikuwa na sababu ya kuficha majina ya wajumbe wanaowakilisha Tanzania kwenye timu hiyo.

“Nimeshangaa kuona serikali imeficha majina ya wajumbe wakati suala la makinikia  linagusa taifa moja kwa moja,”alisema Dk.Kahangwa na kuongeza:

“Wanapaswa kukumbuka kuwa  kampuni hizo zimefanya kazi miaka mingi bila ya kulipa kodi, hivyo wajumbe wa kamati wanapaswa kuwa makini katika mazungumzo yao”.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema:  “Sijajua kwa nini serikali inafanya hivi na ni kwa sababu gani wanafanya hivi hadi tuumizwe ndiyo tunaweka mambo hadharani .

“Ilitakiwa kuwa wazi ili pia kupata sapoti ya taifa siyo wakishaharibu ndiyo wanatangaza ili kupata kuungwa mkono”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Hellen Kijjo-Bisimba alisema: “Mimi jana nilipoangalia picha zile niliona ni wazungu tu kasoro Profesa Kabudi, nikasema au tumekodisha wazungu watusimamie, kumbe kuna watu wetu ambao bado hawajatajwa”.

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye  alisema:  “Jambo hili lingekuwa wazi   tujue jinsi wanavyofanya kazi na kwamba wamefanikiwa au la … kama jambo hili lilianza kwa uwazi basi liishie na uwazi pia”.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba(Jukata),Deus Kibamba, alisema ,“tunapaswa kutambua kuwa  kampuni tunazoenda kujadiliana nazo zinafanya kazi kwa utapeli na   wanajulikana dunia nzima.

“Hivyo basi wajumbe wa kamati kwa upande wa Tanzania wanapaswa kujulikana  wananchi waweze kutoa maoni yao”.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Kwa miaka zaidi ya 50 pamekuwa na uchimbaji wa madini Tanzania ambao ulikuwa ni MWADUI GOLD MINES. Je kuna takwimu gani za mgodi huo? Mwalimu alikataa kabisa kuanzisha migodi mingine na alisema wazi kwamba ni lazima wapate elimu hiyo kwanza na teknologia ya uchimbaji wa madini ndipo tufanye kazi hiyo kwa maana kuwa tujitegemee katika uchimbaji, akasema yaacheni madini yetu yakae huko chini hayaozi (they dont expire)Nachotaka kuuliza kwa watanzania wote ni kwamba tulikuwa na haraka gani ya kuchimba madini yetu na kupata mrahaba wa 3%? Hivi unaweza kuwa na mazao yako shambani ukaweka mkataba na mtu akayavune apeleke sokoni kisha akupatie 3% ya thamani ya mauzo? Sasa tunatangaziwa hasara na ukwepaji wa kodi wa zaidi ya trilioni 420 na kwamba tunafanya mazungumzo nao, yaani unajadiliana na mwizi! Nafikiri serikali ijitathmini vizuri kuhusu madini, ni bora kufunga migodi yote inayoendeshwa na wawekezaji kwa kuwa imekuwa haina tija kwa pato la taifa bali ni hasara na madini yetu yanachukuliwa. Bora tuwaachie wananchi wachimbe kwa sururu wainue kipato chao kuliko kusomewa ripoti za makinikia za ajabu kama hizo, JPM funga migodi yote ya wageni waondoke acha kuwabembeleza, wape wananchi wako wachimbe wenyewe watapata shida, watakufa sana lakini hatimaye watweza kujenga elimu na teknolojia ya uchimbaji

  2. Jamani tujue kuwa madini si kama Miti na Wanyama kwamba ukikata miti unaweza kupanda mwingine au ukawinda wanyama wa porini wanazaliana tena japo pia tunatakiwa kuwa waangalifu katika ukataji wa miti na uwindaji ili tuweze kuweka mizania ya ualisia.
    kwa upande wa madini hali ni mbaya sana, mara unapochimba ka kuchukua madini unapunguza NATIONAL RESERVE iliyopo ardhini na wala haitatokea irudi tena. Economicaly imetusaidia nini kuondosha madini yetu kwa kiwango hicho? Tunakopa wakati tungeweza kuwa na bajeti yetu bila kutegemea msaada wa nchi yeyote!
    Sasa nashauri tuwaachie watanzania wenyewe wachimbe na asiruhusiwe mtu kuuza nje ya nchi bali madini yote yanunuliwe na serikali kwa kuunda agency itakayosimamiwa moja kwa moja na BOT ambayo ndiyo itakayouza nje ya nchi na fedha kuingia serikalini

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles