NAIROBI, KENYA
MGOMBEA urais wa muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga, ameanzisha mashambulizi makali dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta baada ya kususa kujitokeza katika mdahalo wa urais mjini hapa juzi.
Raila alimtuhumu Uhuru kwa woga kwa kushindwa kujitokeza katika mdahalo, ambao Wakenya walijitolea muda wao kuufuatilia.
Akizungumza katikia mkutano wa kampeni huko Meru – siku moja baada ya tukio hilo, Raila alisema kuwa Uhuru aliogopa kuhojiwa na Wakenya kuhusu udhaifu wa uongozi wake kipindi cha miaka mitano.
Alidai kuwa mabilioni ya shilingi yaliibwa huku Uhuru akitazama na hivvyo huu ni wakati wa kumrudisha nyumbani akapumzike.
“Kwa kila shilingi waliyotumia katika nchi hii, waliiba nyingine. Kwa ujumla shilingi bilioni 350 za Kenya zimepotea,” alikaririwa akisema katika mkutano huo.
Raila pia aliulaumu utawala wa Jubilee kwa kutumia chakula ambacho ni haki ya msingi ya raia, kama silaha ya kampeni.
“Wao wanadhani wanaweza kusambaza chakula katika mikutano ya hadhara. Vipi mahali ambako hakuna mikutano au kwa wale ambao hawashiriki mikutano?” alisema na kuhoji Raila.
Awali Raila akiwa Runyenje, Kaunti ya Embu, aliwataka wenyeji wa Mlima Kenya kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 8.
Aliwaamba waliohudhuria mkutano huo kuwa anapenda na kuthamini jamii za Mlima Kenya, ndiyo maana aliungana na Rais mstaafu Mwai Kibaki kuchaguliwa mwaka 2002 kupitia mwavuli wa NARC kama ishara ya ‘mapenzi’ kwa jamii hizo.
“Iwapo ninachukia jamii ya Mlima Kenya je, ningemuunga mkono Kibaki kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2002 kwa kusema ‘yeye tosha’?
“Nilijua yeye anatoka kwa jamii yenu na kwa sababu ninawapenda, nikaamua kumuunga mkono na akaibuka mshindi,” alisema Raila kabla hajaelekea Meru.