NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam inatarajia kusikiliza maombi ya dhamana dhidi ya mfanyabiashara Yusufali Manji anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi Agosti 4, mwaka huu.
Uamuzi huo ulitolewa jana mbele ya Jaji Isaya Arufani baada ya Jamhuri kuomba muda wa kuwasilisha majibu ya hati kinzani.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai maombi ya dhamana waliyapokea na kwa kuwa wana nia ya kuyapinga, wanaomba muda wa kuwasilisha hati kinzani.
Jaji Arufani alikubali kuwapa muda, hivyo Jamhuri itawasilisha Agosti mosi na Manji atajibu Agosti 2 kisha mahakama itasikiliza maombi Agosti 4, mwaka huu.
Manji anawakilishwa na Wakili Joseph Thadayo na Peter Kibatala ambao katika maombi ya dhamana wanaomba mahakama itengue hati ya kumnyima dhamana Manji iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Wanaomba mahakama imwachie Manji kwa dhamana kwa sababu ana matatizo ya kiafya, anasumbuliwa na maradhi ya moyo.
Mawakili hao waliwasilisha vyeti vya daktari kuthibitisha mteja wao ni mgonjwa.
Manji anashtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na upelelezi haujakamilika.
Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 na mihuri.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43). Kesi itatajwa Agosti 4, mwaka huu.
Hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao inadai kuwa Juni 30, 2017 katika eneo la Chang’ombe ‘A, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kwa pamoja washtakiwa walikutwa na askari polisi wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ yenye thamani ya Sh milioni 192.5 ambayo ni mali iliyopatikana kinyume cha sheria.
Katika shtaka la pili, inadaiwa Julai mosi, 2017 huko Chang’ombe ‘A’, washtakiwa hao walikutwa na polisi wakiwa na mabunda manane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ yenye thamani ya Sh milioni 44 mali ambayo ilipatikana isivyo halali.
Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 huko Chang’ombe ‘A’, walikutwa na muhuri wa JWTZ wenye maandishi “Mkuu 121 Kikosi cha JWTZ” bila ya kuwa na uhalali kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Shtaka la nne, inadaiwa kuwa Juni 30, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’, Manji na wenzake hao watatu walikutwa wakiwa na mhuri wenye maandishi “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma” bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Manji na wenzake katika shtaka la tano wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 huko Chang’ombe ‘A’, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maandishi “Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe”, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Katika shtaka la sita, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 katika eneo hilo la Chang’ombe ‘A’, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari “SU 383” ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Katika shtaka la saba washtakiwa wote wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017, eneo la Chang’ombe ‘A’, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari “SM 8573” ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Manji na wenzake wanatetewa na mawakili Hudson Ndusyepo, Malimi Seni na Emmanuel Safari.