BUJUMBURA, BURUNDI
MAANDAMANO yameendelea kwa siku ya tatu jana kwenye mji mkuu wa Burundi, Bujumbura kupinga uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Watu sita wanadaiwa kuuawa na zaidi ya 24,000 kuikimbia Burundi mwezi huu wakiwamo 5,000 walioingia Rwanda mwishoni mwa wiki iliyopita huku hali tete ikiongezeka kuelekea uchaguzi wa urais utakaofanyika Juni.
Watu walionekana wakichoma moto magurudumu ya magari na kuweka vizuizi barabarani huku polisi wakirusha mabomu ya machozi kuwatawanya.
Walioshuhudia walisema milio ya risasi ilisikika na mitaa ilifungwa katika sehemu za mji mkuu.
Maandamano hayo kwa mara ya kwanza yalionekana kusambaa hadi nje ya mji mkuu.
Polisi waliwazuia wanafunzi wa chuo kikuu kwenye mji ulio katikati mwa nchi ambao ni wa pili kwa ukubwa wa Gitega baada ya kujaribu kuandamana kwenda mjini, kwa mujibu wa wakazi wa mji huo.
Maandamano hayo ni makubwa zaidi nchini Burundi tangu kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.
Watu zaidi ya 300,000 walikufa katika vita hiyo katika mapigano baina ya jeshi lililodhibitiwa na Watutsi walio wachache na makundi ya waasi wa Kihutu ikiwamo CNDD-FDD ya Nkrunzinza.
Wanajeshi na polisi wamesambazwa mitaani kukabiliana na waandamanaji ambao wameelezwa na maofisa wa Serikali kama wana mwelekeo wa kuunda makundi ya wanamgambo.
Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon imesema mwakilishi maalumu wa umoja huo, Saidi Djinnit ametumwa nchini Burundi kufanya mazungumzo na Nkurunziza.
UN imesema karibu watu 25,000 wamekimbia nchi hiyo ndani ya majuma mawili yaliyopita, wakihofia kuongezeka kwa ghasia kabla ya uchaguzi mkuu.
Mgogoro huo pia ulitarajiwa kujadiliwa baadaye katika mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
Serikali inawatuhumu waandamanaji kujaribu kuendesha harakati za uasi.
Mawasiliano ya kituo binafsi cha redio nchini Burundi yamesitishwa, likiwa lengo la mamlaka kuzuia taarifa za maandamano kusambaa.
Makamu wa Rais wa Chama Tawala cha CNDD-FDD, Joseph Ntakirutimana amelinganisha redio hiyo na shirika la zamani la utangazaji la Rwanda lililotuhumiwa kuchochea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.