24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi milioni 2.3 wafariki dunia kila mwaka

Dk. Makongoro MahangaNa Debora Sanja, Dodoma
WAFANYAKAZI milioni 2.3 duniani wanafariki dunia kila mwaka kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Duniani.
Alisema takwimu hizo ambazo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kwamba kila sekunde 15 mfanyakazi mmoja anafariki kutokana na ajali au magonjwa duniani kote.
“Aidha zaidi ya wafanyakazi milioni 160 wanapata magonjwa yanayohusishwa na kazi, takwimu ambazo zinatuonyesha kuwa kila baada ya dakika 15 wafanyakazi 153 wanapata magonjwa duniani kote,” alisema.
Dk. Mahanga alisema ajali na magonjwa yanayotokea sehemu za kazi kutokana na kutokuboresha mazingira husababisha gharama kubwa kwa ajili ya matibabu, malipo ya fidia, uharibifu wa mali mbalimbali na kupotea kwa muda wa uzalishaji.
“Suala la kutoa elimu ya kujikinga na ajali na magonjwa yatokanayo na mazingira mabaya ya kazi ni jambo la msingi kwa kuwa jambo linalosababisha ajali kwa kiwango kikubwa linatokana na makosa ya kibinadamu,” alisema.
Aidha alisema mojawapo ya magonjwa yatokanayo na kazi ni maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa.
“Suala la janga la Ukimwi ni sehemu ya usalama na afya mahali pa kazi kwa sababu nguvu kazi inayotegemewa na nchi ndiyo iliyoko kwenye hatari ya kuambukizwa VVU,” alisema.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Selestine Leonard alisema kaulimbiu ya mwaka huu inataka ushirikiano baina ya Serikali, waajiri na wafanyakazi ili kuhakikisha kila mfanyakazi ana uelewa wa kutosha katika suala la kujikinga na ajali kazini.
“Wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira rafiki ya kuwezesha waajiri kutimiza kikamilifu matakwa ya usalama na afya mahali pa kazi,” alisema.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Kujenga Utamaduni wa Kujikinga na Magonjwa na Ajali zitokanazo na Kazi’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles