Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, amefanya mabadiliko ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabus Mwakalukwa, ilieleza kwamba katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Suzan Kaganda, amekuwa Mkuu wa kitengo cha Mafao na Fidia Makao Makuu ya Polisi.
Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Murilo Jumanne ambaye alikuwa kamanda Polisi Mkoa wa Shinyanga.
“Aidha nafasi ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Sylverius Haule, ambaye alikuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi wa Mkoa wa Mara,” ilisema Mwakalukwa katika taarifa yake.
Alisema uhamisho huo ni mabadiliko ya kawaida yanayotokea ndani ya Jeshi la Polisi katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.