MUNICH, UJERUMANI
KOCHA wa klabu ya Bayern Munich, Carlo Ancelotti, amedai kuwa mlinda mlango wa klabu hiyo na timu ya Taifa ya Ujerumani, Manuel Neuer, anaweza kuwa si binadamu wa kawaida ila atakuwa na kompyuta kichwani mwake.
Ancelotti amesema uwezo wa kipa huyo ni mkubwa sana na mchango wake umeifanya klabu hiyo kutwaa mataji sita mfululizo ya Ligi Kuu nchini Ujerumani.
Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ujerumani ambaye amefunga ndoa siku za hivi karibuni, bado ni majeruhi kutokana na kusumbuliwa na goti, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuwa fiti katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu nchini humo dhidi ya Bayer Leverkusen.
“Kwenye kikosi chetu tunayo kompyuta golini ambaye ni mlinda mlango, Manuel Neuer, huyu ni kipa wa pekee kwenye ulimwengu wa sasa, yupo tofauti na makipa wengine ambao nimekutana nao kwa miaka ya hivi karibuni.
“Kuna wakati naweza kusema mchezaji huyo hana mikono, kifua na miguu, lakini anayo ‘keyboard’ ya kompyuta kwenye kichwa chake katika kila mchezo akiingia uwanjani.
“Sina wasiwasi na uwezo wake kwa kuwa mchango wake ndani ya klabu na timu ya Taifa ya Ujerumani umekuwa mkubwa sana, bado ana nafasi kubwa ya kuweka historia ya aina yake kwenye soka,” alisema Ancelotti.
Ijapokuwa kocha huyo amedai kuwa hana wasiwasi na kipa huyo, lakini kwa sasa wapo kwenye mipango ya kuwania saini ya mlinda mlango wa AC Milan, Gianluigi Donnarumma (18).
Hata hivyo, mipango hiyo inaweza kuwa migumu kwa Ancelotti kutokana na AC Milan kuweka wazi kuwa hawana mpango wa kumwacha kipa huyo akiondoka, hivyo wanataka kumuongezea mkataba mpya.
AC Milan wana wakati mgumu wa kuhakikisha mchezaji huyo haondoki kwa kuwa ameweka wazi kuwa anataka kuondoka hana mpango wa kuendelea msimu ujao.