Na MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imeendelea kutoa huduma kwa watoto kwa kuwafungulia akaunti ili waweze kutunza fedha zao zitakazowasaidia hapo baadaye.
Jana Benki hiyo katika viwanja vya ufukwe wa Kawe waliendelea kutoa huduma za kufungulia watoto akaunti katika tamasha la michezo lililoandaliwa na mtangazaji maarufu wa Kituo cha EFM, Dina Mariuos, kwa udhamini wa benki hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo, Mratibu wa Elimu ya Fedha wa NMB, Ryoba Mkono, alisema mpango wa kufungulia akaunti watoto ulianza Agosti, mwaka jana na kwa sasa mwitikio wake umekuwa mkubwa.
Alisema kuna akaunti za aina mbili, ikiwa ni pamoja na NMB mtoto akaunti, ambayo haina ATM kadi na inakuwa chini ya uangalizi wa wazazi kwa asilimia 100, lakini kuna NMB Chipukizi akaunti, hii ni kuanzia miaka 13 -18, mtoto anapewa kadi na kujitunzia fedha zake yeye mwenyewe.
Alisema huduma ya NMB Chipukizi akaunti mtoto anatunza fedha zake na anaruhusiwa kutoa kuanzia kiwango cha Sh 5,000 hadi 50,000 na akitoa mzazi wake anatumiwa ujumbe wa meseji kwamba zimetolewa fedha.
“Huduma hii ya watoto ni nzuri sana na huwasaidia watoto kujifunza jinsi ya kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye, lakini NMB tunazunguka mashuleni kuweza kutoa elimu hiyo kwa walimu na wanafunzi wao pia,’’ alisema Mkono.
Aliongeza kuwa, mzazi anaweza kumuwekea mtoto wake fedha bila kwenda kwenye tawi lolote akatumia simu na kuweka fedha katika akauti husika.