Na HARRIETH MANDARI – GEITA
WAKAZI wawili wa Kitongoji cha Bugande kilichopo Kijiji cha Mharamba mkoani Geita, wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa ni bomu.
Waliofariki katika tukio hilo ni William Jija (35) na Dennis Faida (5) na aliyejeruhiwa ni mtoto Emmanuel Juma.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, alisema kitu hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu kiliokotwa na watoto karibu na makazi ya watu na walikipeleka nyumbani kwao wakitarajia kuuza kama chuma chakavu maarufu kwa jina la ‘mabembelejojo’.
Akisimulia jinsi tukio lilivyotokea, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bugande, Paulo Gerald, alisema mlipuko ulitokea Juni 30, mwaka huu saa tisa alasiri na watoto Denis Emmanuel walikuwa wakicheza karibu na nyumba ya Jija.
Alisema watoto hao waliokota chuma hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu na kukipeleka kwa Jija ambaye baada ya kukipokea alifyatua kichuma kilichokuwa kwa juu na baada ya muda kidogo lililipuka na kusababisha kifo chake na cha Dennis aliyekuwa pembeni yake.
“Nilipoona moshi unatoka kwenye lile chuma nikakimbia halafu wakati nakimbia kulilipuka moto mkubwa,” alisema Emmanuel aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Naye muuguzi wa Zahanati ya Nzela, Hawa Ismail, alisema walimpokea majeruhi huyo akiwa katika hali mbaya na kumpatia huduma ya kwanza na kwa sasa anaendelela vizuri.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho baada ya tukio hilo, Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya Geita, Akisibomana Mseke, aliwatahadharisha wananchi hao kuwa makini na vitu wasivyovijua na kuepuka kuokota vitu vinavyotia shaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi, aliwataka wananchi kutoa taarifa katika ofisi za vijiji na kata pale watakapoona vitu vinavyotia shaka.
“Nchi yetu ni ya amani, hivyo wapo wageni wanaoingia kinyemela na kati yao inawezekana kabisa wanakuja na silaha kama hizo, hivyo inapotokea mnaona mgeni yeyote msiyemfahamu toeni ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa viongozi wenu wa vijiji,” alisema.
Alisema upo umuhimu wa kuanzisha tena ulinzi wa sungusungu uliosaidia kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Kama tunavyojua hatuna polisi wa kutosha kulinda vijiji na vitongoji vyote katika nchi yetu, hivyo ulinzi wa sungusungu haukwepeki, ni lazima utaratibu uanzishwe ili ulinzi huo urudishwe kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita,” alisema Kapufi.