MAHABUSU CHUNGU KWA VIGOGO 29

0
624

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

KUFIKISHWA mahakamani kwa viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa tuhuma tofauti, zikiwamo za utakatishaji fedha, limeongeza idadi ya vigogo wa kada tofauti wanaosota rumande katika magereza mbalimbali hapa nchini, yakiwamo Keko na Segerea yaliyopo Dar es Salaam.

Viongozi wa TFF waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Alhamisi wiki hii, ni Rais Jamal Malinzi, Katibu Celestine Mwesiga na Mhasibu Nsiande Mwanga, wanaotuhumiwa kwa makosa 28, yakiwamo matatu ya utakatishaji fedha na kughushi nyaraka walipofanya malipo.

Ndani ya tuhuma hizo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 25 na kesi yake itatajwa tena mahakamani hapo Julai 3, mwaka huu.

Mbali na vigogo hao wa TFF, vigogo wengine wanaosota rumande ni Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kwa jina la Kaburu ambao nao walifikishwa mahakamani hapo kwa makosa ya kuhamisha kinyemela Dola 300,000 za Marekani na kutakatisha fedha.

Aveva na Kaburu walisomewa kwa mara ya kwanza mashitaka yao ikiwamo kutakatisha fedha na kesi yao imeahirishwa hadi Julai 13, mwaka huu.

Kigogo mwingine anayeendelea kusota rumande ni Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na maofisa wawili waandamizi wa Benki ya Stanbic Tanzania ambao ni Sioi Solomon aliyewahi kugombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki mwaka 2012 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya baba yake aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari, kufariki dunia na Shose Sinare aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali likiwamo la utakatishaji wa fedha na kwa mara ya kwanza walisomewa mashtaka yao Aprili, mwaka jana katika mahakama hiyo.

Mashtaka mengine wanayotuhumiwa kina Kitilya ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo na kujipatia isivyo halali Dola milioni sita za Marekani sawa na Sh bilioni 12 pia katika tarehe tofauti kati ya Agosti, 2012 na Machi 2013 jijini Dar es Salaam walipanga kwa ushirikiano na watu wengine kujipatia fedha kutoka serikalini kwa udanganyifu.

Vigogo wengine wanaosota rumande baada ya kufikishwa mahakamani hapo ni wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na mwenzake James Rugemalira wanaodaiwa kuhusika na uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)/Pan Africa Power (PAP) na Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, mwaka huu na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi, kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu na kutoa nyaraka za kughushi na kupelekwa rumande hadi Julai 3, mwaka huu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Kigogo mwingine anayeendelea kusota rumande ni Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki) maarufu kama Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed.

Sheikh Farid na wenzake saba wameshtakiwa kwa makosa ya ugaidi na wameendelea kusota rumande tangu mwaka 2012 wakitokea Zanzibar.

Mwingine anayeendelea kusota rumande ni Wakili Median Mwale na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka 42, likiwamo la utakatishaji fedha.

Wakili Mwale na wenzake walisomewa mashtaka hayo Januari 21, mwaka juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kigogo mwingine anayesota rumande ni raia wa China, Yang Feng Glan, anayekabiliwa na kesi ya biashara ya pembe za ndovu.

Yang ambaye ni maarufu kwa jina la Malkia wa Pembe za Ndovu, anasota rumande tangu mwaka 2014.

Pia mtuhumiwa Yusuph Ali maarufu kwa jina la Mpemba naye anasota rumande kwa takriban miezi saba sasa kutokana na mashtaka ya biashara ya pembe za ndovu.

Mpemba na wenzake wawili, Pius Kulagwa na Ahmed Nyagongo, wanakabiliwa na mashtaka manne ya kukutwa na pembe za ndovu kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara.

Kigogo mwingine anayeendelea kusota rumande tangu mwaka juzi ni mfanyabiashara Ali Khatibu Haji maarufu kwa jina la Shikuba, anayekabiliwa na mashtaka ya kuuza dawa za kulevya.

Shikuba aliyekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kupelekwa rumande katika Gereza la Mkoa wa Lindi kwa sasa na mwenzake mmoja wamepelekwa kushtakiwa nchini Marekani.

Pia mfanyabiashara Mharami Mohamed Abdallah maarufu kwa jina la Chonji, naye anaendelea kusota rumande tangu mwaka 2014 baada ya kukutwa na dawa za kulevya katika makazi yake yaliyopo Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here