25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA: HAKUNA MSAMAHA KWA WABADHIRIFU WA MALI ZA USHIRIKA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

Na Mwandishi Wetu – Dodoma


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali haitamsamehe mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu wa mali za ushirika.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD).

“Tutachukua hatua kali kwa wezi wa mali na fedha za ushirika na tunaendelea kufanya usafi wa wabadhirifu hadi tupate viongozi waadilifu,” alisema.

Majaliwa alisema miongoni mwa changamoto zinazoukabili ushirika hapa nchini ni wizi na ubadhirifu wa rasilimali zake unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waaminifu.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kutoheshimu miongozo ya vyama vyao na kujifanyia mambo kwa masilahi yao binafsi.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake na kuweka mazingira rafiki ya kustawisha ushirika ili kutoa fursa ya kushamiri na kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi yao.

“Haikubaliki hata kidogo kuona sekta hii inayosadifu maisha ya Mwafrika haimnufaishi ipasavyo, hivyo naelekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika hapa nchini ihakikishe kuwa vyama vya ushirika vinaendeshwa kisayansi na kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Pia alizielekeza kamati za ushauri za mikoa na wilaya ziingize ajenda ya maendeleo ya ushirika kama moja ya ajenda muhimu inayopaswa kujadiliwa na kuwekewa maazimio ya utekelezaji.

Aliagiza masuala yote yanayohusu ushirika wa kilimo lazima yaratibiwe na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Awali, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alisema wataendelea kuchukua hatua kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaobainika kufanya ubadhirifu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles