27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

RAMADHANI BADO HAIJAISHA MJUE…

BADO tupo kwenye mwezi mzuri sana. Mwezi mwema ambao hujulikana pia kama mwezi wa toba – Mwezi Mkutukufu wa Ramadhani.

Leo ikiwa ni Ramadhani 29, tunachosubiri ni mwandamo wa mwezi, kisha mialiko ya pilau na biriani za Sikukuu ya Eid-Elfitri.Utulivu umekuwa mkubwa sana kwa mwezi wote huu.

Ni mwezi wa funga kwa Waislamu, lakini kwa hadhi ya mwezi wenyewe na maana yake, hujitokeza tu mambo yanabadika. Wale waliokuwa wakifanya maovu, wamekuwa watulivu.

Sio kwa Waislamu pekee na siyo kwa wanaofunga pekee, bali jamii nzima imetulia kabisa. Kwa sababu huu ni uwanja wetu siye vijana, nikisema kwamba ni kweli kuwa hata zile amshaamsha zetu kwa mwezi huu tulizituliza, naamini hakuna atakayenibishia.

Watu wameishi utaratibu mpya kabisa wa maisha kwa kipindi hiki. Ni jambo zuri na la kumshukuru Mungu. Wapo masela zangu ukikutana nao kipindi hiki na kuwauliza vipi hawaonekani kwenye mitaa yao ya matukio, watakujibu hapana huu ni mwezi wa haki.

Wanafanya vyema na hawakosei kwa hakika, lakini kama vijana tunatakiwa kujifunza zaidi ya hapo. Hatutakiwi kuacha mabaya kwa ajili ya mwezi huu tu.

Huenda leo usiku mwezi ukaonekana, kesho ikawa Idd vinginevyo keshokutwa Jumatatu. Sasa yale mabaya tuliyoyasahau vijana tunaibuka nayo kwa upya.

Ukienda nyumba za wageni unakuta zimejaa asubuhi-asubuhi! Unajiuliza inawezekana vipi nyumba ya wageni iliyopo Tandale ijae saa tatu asubuhi? Kumbe kuna watu walipisha mwezi wa Ramadhani.

Hayo ni makosa makubwa sana. Tunapaswa kuishi kwa hofu na kujua kuwa Mungu yupo siku zote kwenye maisha yetu. Nasema zaidi na vijana kwa sababu ndiyo taifa la leo.

Sisi ndiyo wenye nguvu ya kuharibu au kutengeneza taifa zuri. Kama vijana tujitazame upya, yale yasiyo na tija tuyaache. Tufanye yale yaliyo mema na yenye maana kwenye maisha yetu.

Kwani starehe mwisho wake nini? Zitakusaidia nini? Hakuna cha maana. Mwisho washkaji nawatakieni heri ya Sikukuu ya Idd na tuburudike kwa kiasi.

Nawakumbusha tena, starehe zisizo na maana tusizipe nafasi, maana unaweza kuwa mtulivu kwa mwezi mzima na ukapata thawabu nyingi lakini ukaharibu zote kwa tukio la siku moja tu.

Ramadhani inapaswa kuwa kwenye maisha yetu siku zote. Kwaheri Mwezi Mkutukufu wa Ramadhani, nawatakieni heri na fanaka Waislamu wote nchini sikukuu njema. Mialiko bado haijafungwa, nitakuja na pilipili na ndizi mbivu kabisa.

Mungu awabariki sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles