25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UKIAMBIWA HUWEZI WAAMBIE WAKUAMBIE RANGI ZA WANAOWEZA!

Na ATHUMANI MOHAMED

LAZIMA utumie akili nyingi sana ili uweze kufanikiwa maishani vinginevyo utabaki kuwa msindikizaji tu. Lakini wakati ukifukuzia ndoto zako, kumbuka kuwa unaishi kwenye jamii ambayo imetofautiana tabia na mitazamo.

Kwa mtindo huo basi inakupasa kuishi kwa akili na maarifa ya ziada ili kuweza kushinda changamoto mbalimbali za kimaisha. Ukiishi kwa taratibu za kawaida, za kuamka asubuhi na kwenda kazini, kisha kupitia kwa marafiki na baadaye nyumbani, kisha asubuhi nyingine imefika, utabaki kuwa msindikizaji kwenye maisha yako.

Kwenye jamii yetu wapo watu ambao kazi yao ni kukatisha wengine tamaa.Kila ukihangaika kufanya hivi, wao wanakuambia vile. Mfano unataka kuanzisha biashara fulani, unamwuliza mtu unayemwamini kwamba una wazo na unahitaji usaidizi wake.

Wengi wataishia kukukatisha tamaa, kwamba jambo hilo haliwezekani. Mabingwa wa kukatisha wengine tamaa huenda mbali zaidi na kukutolea mpaka mifano ya watu wakubwa walioshindwa wakati wewe ukitaka kupitia njia hiyohiyo.

Ukikutana na watu wa namna hiyo maishani mwako na ukawapa nafasi hiyo kichwani mwako ni wazi kuwa utaishia kuwa masikini maishani mwako.

 

ISHI MAISHA YAKO

Kuwa makini na maisha yako. Siri kubwa ya kuibuka mshindi ni kuacha kuwaamini watu wote kisha ujiamini wewe mwenyewe. Akili yako ina maana zaidi ya mwingine yeyote maana wewe ndiye unayepanga unachotaka kufanya na malengo yapo kwenye mikono yako.

Usiwaogope wakatishaji tamaa, lakini unachotakiwa kufanya ni kuwasikiliza na kuwaacha kama walivyo. Sogea mbele kwa matumaini ukiiamini zaidi akili yako.

Mwenye uchungu wa kweli na maisha yako ni wewe mwenyewe. Mwenye hasira ya kweli na maumivu ya umasikini wako ni wewe mwenyewe. Hata mzazi wako hawezi kuwa na maumivu makali juu ya maisha yako kama wewe mwenyewe.

Umia mwenyewe. Fikiria njia za kupenya ili uweze kuibuka mshindi.

 

MAGUMU NDIYO USHINDI

Historia za matajiri wengi ulimwenguni zinaonyesha kuwa walianzia sifuri. Kuna matajiri wachache sana ambao utajiri wao umetokana na urithi wa wazazi wao.

Wengi ni wale ambao walianzia sifuri. Walianza kwa kubuni vitu vikubwa wakitokea masikini kabisa. Wapo wafanyabiashara wakubwa hapa nchini ambao hawana elimu kubwalakini wamefanikiwa.

Wapo matajiri wakubwa ambao walikuwa wakifeli darasani lakini sasa hivi ni mabilionea wakubwa. Hii maana yake nini? Inamaanisha kuwa elimu ya darasani wakati mwingine si kigezo cha mafanikio ya kimaisha.

Unatakiwa kufikia zaidi nje ya boksi ili uweze kuwa na mafanikio na kuwashangaza wale ambao siku zote huwakatisha tamaa wengine. Kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba wale wanaokatisha tamaa wenzao, huwa hawana vya maana, ila kwao ni burudani tu kuwakatisha tamaa wengine ili wote muonekane mmekosa!!!

 

ULIZIA RANGI

Kwenye kichwa cha mada yetu hapo juu, nimesema wanaokuambia haiwezekani waambie wakuonyeshe rangi za wanaoweza. Hapo namaanisha kwamba utajiri ni haki ya kila mtu, jambo la msingi ni kujitambua na kuzitumia fursa zinazokuja mbele yako bila kupoteza.

Fanya vitu vingi kadiri unavyoweza. Kwa mfano nikijitolea mfano mimi binafsi. Sina elimu kubwa sana, lakini kwa mazoea yetu Waafrika, mtu kuwa na degree (ambayo ninayo), anaonekana anapaswa kufanya kazi za ofisini.

Kwangu mimi nimesema no! Nafanya biashara nyingi sana kwa wakati mmoja nikiwa na mategemeo ya kubadilisha maisha yangu. Nimeshasahau kama nina degree. Mwaka wa nne sasa nafanya ujasiriamali.

Wiki iliyopita nilikuwa nazungumza na vijana mahali fulani kule Arusha, nikawaeleza ushuhuda huu, wakashangaa. Lakini unajua nini? Wapo rafiki zangu wengi waliotuma CV zao kwenye kampuni mbalimbali tangu tumemaliza chuo na hawajaitwa hata kwenye usaili mpaka leo. Tutafananaje? Ni usiku na mchana.

Ninawatakieni mema. Mungu akipenda tutakutana wiki ijayo katika mada nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles