Na MANENO SELANYIKA
-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Marco (54), kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh 13,900,000 baada ya kukiri mashtaka nane, likiwamo la kuishi na kufanya kazi hapa nchini bila kibali.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, baada ya Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma, kumsomea mashtaka yake pamoja na maelezo ya awali ambapo mtuhumiwa alikubali.
“Kwa kuwa umekiri makosa yote kwa kuzingatia sheria na kanuni, mahakama hii inakutia hatiani, hivyo unatakiwa kulipa faini shilingi milioni 13,900,000 au uende jela miaka mitano na kwamba ni haki yako endapo hujaridhika na uamuzi huo ukate rufaa uende katika ngazi nyingine ya juu,” alisema Nongwa.
Kagoma alidai mbali na kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma kwa mshtakiwa, pia aliomba mahakama impatie adhabu kali ili iwe fundisho kwake pamoja na watu wengine wanaoishi nchini bila kufuata taratibu za Jamhuri ya Muungano.
Baada ya maelezo hayo kutolewa, mtuhumiwa huyo alipewa nafasi ya kujitetea na akisaidiwa na Wakili wake, Aloyce Komba, aliomba adhabu itakayotolewa kwa mteja wake isiwe kubwa kwa sababu amekiri makosa, hivyo imepunguza gharama kwa mahakama kuita mashahidi.
“Adhabu utakayoitoa ioneshe kwamba haki siyo tu kuwa inatendeka, bali imetendeka kwa sababu mteja wangu ni mara ya kwanza hajawahi kuvunja sheria ya Jamhuri, hususan ya kijinai kama upande wa mashtaka walivyodai.
“Ni mwajiriwa wa TBS kwa kipindi kirefu, hivyo ni mwadilifu na mbunifu wa kazi, hajawahi kutoa siri wala si msaliti, hivyo mahakama hii tukufu imfikirie adhabu, hasa katika shtaka la nane,” alidai.
Komba aliendelea kudai kuwa, japo mteja wake ana hadhi ya ukimbizi, pia ana mke na watoto wanne wanaosoma, wazazi wake ni wazee hawajiwezi wanamtegemea na aliiomba mahakama izingatie hayo katika adhabu hiyo.
Awali, katika hati ya mashtaka iliyosomwa na Kagoma, alidai kuwa Mei 19, mwaka huu, huko Kinondoni katika Ofisi za Uhamiaji, Marco akiwa ni raia wa Burundi alikutwa nchini bila kuwa na kibali cha kumwezesha kuishi.
Katika shtaka jingine, amedaiwa kuwa siku hiyo alikutwa akifanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya kazi hapa nchini.