SERIKALI KUSHIRIKISHA NCHI NYINGINE KUDHIBITI RUSHWA

0
511

Na PATRICIA KIMELEMETA

SERIKALI imeahidi kushirikiana na nchi zilizofanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuhakikisha inaimaliza.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, katika mkutano wa mapambano dhidi ya rushwa ulioshirikisha wadau kutoka nchi zaidi ya tano, ikiwamo Romania, Uingereza, Botswana, Madagascar, Swaziland na Georgia.

Kairuki alisema kuna baadhi ya nchi zimefanikiwa katika mapambano hayo, ikiwamo Madagascar na Georgia, hivyo ni wakati wa kuhakikisha Serikali inashirikiana nao.

“Kuna baadhi ya nchi zimefanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo basi, Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha rushwa inakwisha,” alisema.

Kairuki alisema kutokana na hali hiyo, Serikali itahakikisha sekta ya ununuzi na miradi ya maendeleo inasimamiwa vizuri, ili zifanye kazi bila ya kuwapo kwa mazingira ya rushwa.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, alisema ameshauriana na Benki ya Dunia (WB) ili kuangalia mikakati ya utekelezaji wa kupambana na rushwa nchini.

Katika mikakati hiyo, alisema watashirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo sekta muhimu na asasi za kiraia na itasaidia katika utekelezaji wake.

Kuhakikisha mikakati hiyo inafanikiwa, alisema watakusanya maoni na kuchukua mawazo mbalimbali yaliyotolewa na viongozi waliohudhuria mkutano huo, ili waweze kuyafanyia kazi.

“Lengo letu ni kumaliza tatizo la rushwa  nchini, ambapo katika utekelezaji wake tutashirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo sekta muhimu na asasi za kiraia ili kuhakikisha tunafanikiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, alisema mfumo uliopo unachangia kuendelea kwa vitendo vya rushwa.

Waitara alisema kuna baadhi ya watu wanatajwa kujihusisha na rushwa, lakini Serikali inashindwa kuwachukulia hatua kutokana na kuwasaidia katika shughuli mbalimbali, ikiwamo kampeni.

“Huku kwenye siasa rushwa imetawala kwa kiasi kikubwa, lakini watu hao wanashindwa kuchukuliwa hatua kwa sababu waliwasaidia viongozi kuingia madarakani,” alisema.

Waitara alisema, ifike wakati Serikali ibadili mfumo wa kulindana na kuwashughulikia watu wote wanaojihusisha na rushwa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here