29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mzee Moyo afukuzwa CCM

hassan-nassor-moyoNA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimemfukuza uanachama mmoja wa waasisi wa chama hicho Visiwani, Mzee Hassan Nassor Moyo.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja, Aziza Iddi Mapuri katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari mjini hapa.

Mapuri alisema Mzee Moyo anadaiwa kukisaliti chama hicho kwa kukiuka maadili na kutoa matamshi yasiyokubaliana na sera za chama chao.

Alisema Mzee Moyo alitumia majukwaa ya siasa katika mikutano iliyoandaliwa na Chama Cha Wananchi (CUF) kuisaliti CCM huku akijua kuwa yeye ni kiongozi wa kutolewa mfano.

Kwa mfano, alisema, Aprili 30, 2014 katika mkutano ulioandaliwa na CUF katika Viwanja vya Kibandamaiti Unguja, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alimsimamisha Mzee Moyo jukwaani, ambaye naye alitamka kwamba Serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari wote.

Alisema katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Tibirinzi Pemba Februari 9, 2014, Mzee Moyo alijitambulisha kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano kutoka CCM jambo.

Alisema CCM haimtambui Moyo kuwa na wadhifa wa aina hiyo.

Mapuri alisema baada ya kutafakari kwa kina chama hicho kilibaini kwamba kiongozi huyo anaongoza kwa upotoshaji wa hali ya juu na hafai kuendelea kuwa mwanachama wa chama hicho.

“Wakati akihutubia kongamano la CUF katika ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, alibeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kwamba mkataba wa Muungano wa Aprili 26, 1964, haujulikani ulipo na wabunge wa Bunge la Katiba walikuwa hawajui wanachokifanya na kwamba wameisaliti Zanzibar.

“Kutokana na matukio yote hayo na matamko anayoyatoa Mzee Moyo amepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni mfano wa kutegemewa kwa wazee na vijana,” alisema Mapuri.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa jijini Tanga kwa mapumziko, Mzee Moyo alieleza kushitushwa na taarifa za kufukuzwa uanachama katika CCM akisema hakuwa na taarifa hizo.

Mazungumzo ya MTANZANIA na Mzee Moyo yalikuwa hivi:

MTANZANIA: Shikamoo Mzee kuna taarifa umefukuzwa uanachama wako ndani ya CCM, umepokeaje taarifa hizo?

Mzee Moyo: Eeeh, sina taarifa, unasemaje? Sijapewa barua!

Hata hivyo MTANZANIA ililazimika kukata simu kumpa muda Mzee Moyo kutafakari.

Baada ya muda kupita alipigiwa tena simu ambako alisema hajutii uamuzi huo kwa sababu yeye hakuzaliwa kuwa mwanachama wa CCM daima.

“Mimi sijutii kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi kwa sababu sikuzaliwa kuwa mwanachama wa chama hicho milele, Natofautiana na CCM katika mambo mbalimbali likiwamo suala la muundo wa muungano,” alisema.

Katika siku za hivi karibuni, Mzee Moyo katika mikutano ya siasa ambayo amekuwa akialikwa na CUF amekuwa akitamka bayana kwamba Muungano wa Serikali mbili umepitwa na wakati na ipo haja kwa Zanzibar kuwa na mamlaka kamili.
Mzee Moyo (81) ni miongoni mwa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Vilevile, siku chache baada ya Muungano mwaka 1964 Mzee Moyo aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Baadhi ya nyadhifa alizowahi kutumikia katika Serikali ya Muungano ni pamoja na mbunge na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 1977.

Katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amewahi kushika nyadhifa mbalimbali tangu mwaka 1964 na kufanya kazi kwa karibu na Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume kwa kuongoza Wizara ya Kilimo kwa muda mrefu akifanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani ya Chama cha ASP ya kumgawia kila mwananchi ekari tatu za ardhi,

Mzee Moyo ni miongoni mwa viongozi wa mwanzo wa Chama Cha Mapinduzi baada ya kuzaliwa mwaka 1977.

Alikabidhiwa kadi namba saba katika sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles