31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa athibitisha ubora wa afya yake

lowassa 1Na Asifiwe George, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowasa, jana alithibitisha kwa vitendo kuwa afya yake iko safi baada ya kutembea umbali wa kilomita tano kwa miguu kwenye matembezi ya kupinga mauaji ya albino nchini.
Kwa muda mrefu, Lowassa ambaye ni mmoja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, amekuwa akidaiwa kuwa na matatizo ya afya na kuwa hawezi kuhimili mikimiki ya kampeni na shughuli nyingine zinazohitaji nguvu.
Lakini matembezi ya jana yaliyoongozwa na Lowassa kuanzia Uwanja wa Taifa wilayani Temeke mpaka viwanja vya TCC Chan’gombe na kutumia dakika 25, yamedhihirisha vinginevyo.
Matembezi hayo yalianzia barabara ya Mandela, Kilwa kupitia Temeke Mwisho, Wiles, Temeke Hospitali, Chang’ombe Polisi, Kiwanda cha Bia cha Serengeti na kuhitimishiwa viwanja vya TCC.
Akizungumza baada ya kuhitimisha matembezi hayo yaliyoandaliwa na kikundi cha Temeke Family Sport Club, Lowassa alisema hakushiriki matembezi hayo kwa lengo la kufanya siasa bali ni kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete katika vita dhidi ya mauaji ya albino.
“Hapa sikuja kufanya siasa, nimekuja kumuunga mkono Rais Kikwete katika suala la kupambana na kupinga mauaji ya albino,” alisema Lowasa.
Lowassa aliiomba Serikali kuongeza jitihada katika uhamasishaji na kupinga mauaji hayo.
“Wananchi nao wanalo jukumu la kushiriki na kulinda ikiwa ni pamoja na kupinga mauaji ya albino na si kuiachia Serikali pekee.
“Tunatakiwa tutambue albino ni sawa na watu wengine na wasitengwe kwa sababu nao wana haki ya kuishi kama watu wengine.
Akizungumzia ajali za barabarani, alisema nyingi zinatokana na uzembe wa madereva wanaopenda kuendeshwa kwa mwendo kasi, hivyo akawataka abiria kukemea mwendo kasi wanapokuwa ndani ya vyombo vya usafiri.
Mwenyekiti wa Temeke Family Sport Club, Hassan Muharami alisema katika matembezi hayo wameshiriki zaidi ya watu 10,000 kutoka vilabu 100.
Alisema lengo la kikundi chao ni kusaidiana katika mambo ya jamii, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na makundi hatarishi kama vile utumiaji wa dawa za kulevya na ujambazi.
Alisema matemebezi hayo yameanza katika jiji la Dar es Salaam na baada ya hapo yatafanyika katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki na kuwalinda albino.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles