Na CHRISTOPHER MSEKENA
MWIMBAJI staa wa muziki wa asili nchini, Saida Karoli mwishoni mwa mwaka jana alirudi kwa kishindo kwenye ulimwengu Bongo Fleva, baada ya wasanii watatu kutumia vionjo vya nyimbo zake katika kazi zao mpya zilizofanya vizuri zaidi.
Septemba 18, mwaka jana Diamond Platnumz aliachia ngoma yake aliyomshirikisha Rayvanny inayoitwa Salome ambayo ina vionjo vya mdundo na baadhi ya mistari kutoka kwenye Maria Salome (Chambua Kama Karanga) ulioimbwa zamani na Saida Karoli.
Wimbo huo ulipata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kumrudisha upya Saida kwenye ulimwengu wa biashara ya muziki pia ulichezwa kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kufanya watu ambao walikuwa hawamfahamu Saida wapate kumtambua.
Mbali na hilo, ngoma hiyo ilitengeneza fedha kupitia Youtube ambapo mpaka sasa video hiyo imetazamwa na watu zaidi ya milioni 16.2.
Novemba 23, mwaka jana, bosi wa Classic Music Group (CMG), Darassa alikuwa ni msanii wa pili kutambulisha wimbo wake aliomshirikisha Ben Pol unaoitwa Muziki ukiwa na vionjo vilivyochotwa kwenye ngoma ya Saida Karoli, Chambua Kama Karanga.
Maajabu ya wimbo huo yanafahamika, sina wasaa mpana wa kuyaelezea hapa ila Muziki ni moja ya ngoma kali zilizompa mafanikio Darassa ya kifedha na kisanaa ambapo hiyo ndiyo video yake ya kwanza kutazamwa na watu milioni 8.3 huku jina la Saida Karoli likiendelea kutamalaki kwenye vinywa vya mashabiki kwa wimbo wake kutumika kwenye kazi kubwa kama ile.
Desemba 17, mwaka huohuo jina la Saida Karoli liliendelea kugonga vichwa vya habari za burudani mara baada ya staa wa Bongo Fleva, Belle 9 kuachia wimbo unaoitwa Give It To Me aliomshirikisha G Nako, huku ukiwa na vichombezo kutoka kwa mkongwe huyo wa muziki wa asili.
Ngoma ya Give It To Me ni kazi ya kwanza kwa Belle 9 kutazamwa na mashabiki wengi ambapo mpaka sasa ina watazamaji zaidi ya milioni 1.
Hayo ni mafanikio kwake Belle 9 na Saida ambaye kwa kitambo kirefu alikuwa kimya. Mfululizo wa nyimbo hizo tatu kutoka kwa Diamond Platnumz, Darassa na Belle 9 ulimuibua upya Saida Karoli ambapo alipata nafasi ya kutumbuiza kwenye maonyesho kadhaa na kuvuta mkwanja mrefu.