UCHAWI KWENYE SANAA NI UBUNIFU

0
1050

KWA maisha yetu ya kila siku, hakuna cha kushangaza unaposikia fulani anajihusisha na mambo ya kishirikina. Ni stori za kawaida. Utasikia juzi Dula alimwendelea demu wake wa Manzese kwa sangoma ili azidishe mapenzi.

Kesho usishangae kusikia kuwa Julius naye amesafiri kwenda mkoani kumuona mtaalamu wake ili ampe dawa ya biashara.

Siyo kitu cha kushtua kuambiwa kuwa mama fulani muuza chakula, ana wateja wengi zaidi kwa sababu amepewa dawa na babu ambayo huvutia wateja. Ni stori za namna hiyo.

Nimesema siyo za kushangaza, lakini kwangu mimi siamini kabisa hayo mambo ingawa najua yapo. Sikatai kwamba hakuna watu wanaokwenda kwa wataalamu, lakini tujiulize wanachokifuata wanakipata kweli?

Mimi naona kama kiini macho tu. Hivi kweli mama lishe aende kwa mganga apewe dawa ya kismati, halafu apike chakula cha hovyo, atapata wateja kweli kwa sababu ati ana dawa ya biashara? Thubutu!

Hakuna kitu kama hicho. Kama huna ubunifu kwenye unachokifanya hesabu maumivu tu. Huwezi kupata wateja katu. Utatembea kwa waganga wote, lakini vitakudodea! Huo ndiyo ukweli ambao wengi wanaoshiriki kuhangaika huko kwa wataalamu hawapendi kusikia.

Sasa hizo stori zimehamia kwenye sanaa. Baadhi ya wasanii wameweka mategemeo yao kwa waganga wa kienyeji. Ati wakienda huko na kufanyiwa vidawa vya hapa na pale, ati watapata ngekewa na kupendwa.

Utasubiri sana. Kuna wakati wasanii fulani waliwahi kuripotiwa kugongana kwa sangoma. Mbona ilikuwa balaa. Ilikuwa patashika, nguo kuchanika lakini mwisho wa siku wakakubaliana iwe siri, wakasahau dunia haina siri. Mchezo ukavuja.

Wako wapi? Hakuna kitu. Leo kuna wasanii wanafanya vizuri, wasanii wenzao wanaamini eti ni nguvu ya dawa za kienyeji. Si kweli. Ni suala la juhudi na kujituma.

Kama kweli unataka kuwa juu kwenye kazi zako za sanaa, pambana na ubunifu. Hakikisha kila siku unakuwa mpya. Ujanja ni kuwa mbunifu. Sasa kama wewe kila siku unakesha klabu, huna muda wa kuangalia wenzako wanafanyaje, itawezekanaje kutoboa?

Utaishia kulalamika kwamba wenzako wanatumia nguvu ya ndumba huku wewe ukiendelea kudoda. Endelea kubaki na mawazo yako mgando, utakuja kuona matokeo yake.

Kama huna ubunifu utabaki hapohapo ulipo siku zote. Sumbua kichwa chako, jitahidi kuwa mbunifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here