25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

LUKUVI: WAFANYAKAZI CDA WAMEFICHA VIWANJA 34,000

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA


WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amedai kuwa waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) wameficha zaidi ya viwanja 34,000.

Lukuvi ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CDA kwa miaka kadhaa, pia amesimulia jinsi wabunge wanne walivyotapeliwa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli aliifuta mamlaka hiyo na shughuli zake kuhamishia Manispaa ya Dodoma.

Akizungumza mjini hapa jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Chama cha Wapima Ardhi Tanzania (IST), Lukuvi alisema viwanja vilivyopimwa Manispaa ya Dodoma vilikuwa 60,000, lakini vilivyoonekana ni 26,000 tu huku 34,000 vikiwa vimefichwa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi, Serikali imegundua wafanyakazi wengi wameiba viwanja na kuviuza kwa watu wengine.

Lukuvi alisema kulikuwa na utaratibu wa wafanyakazi wa CDA kuuza viwanja kwa njia za panya kwa Sh milioni 5, kisha mhusika kupelekewa nyaraka mahali alipo.

Alisema kuna wabunge wanne waliuziwa viwanja kwa kutoa Sh milioni 5, lakini kesho yake rais akaivunja mamlaka hiyo na kujikuta wakitapeliwa.

Lukuvi alisema wabunge hao walikwenda kumlilia wakitaka kurudishiwa fedha hizo, lakini jambo la kushangaza hawakuwa na ‘invoice’ ya aina yoyote.

“Sasa wapo watu ambao wamewalipa hizo milioni tano, halafu kesho yake ikala kwao, Mheshimiwa Rais kaifuta CDA, ndiyo wanakuja kusema kwangu, watalipwaje? Nimewaambia nipeni risiti wanasema hawana. Nitawapa kitu gani? Majina ninayo,” alisema.

Alisema wale wote walioiba viwanja hivyo vitawatokea puani, kwani Serikali tayari inayo ripoti nzima juu ya wizi huo.

 “Serikali inakosa mapato, sasa tunataka viwanja vipimwe vingi ili tuweze kujiingizia mapato,” alisema.

Aidha Lukuvi alimbana aliyekuwa Mpimaji Mkuu wa CDA, Frank Mkomochi ambaye alikuwapo katika mkutano huo, akidai kuwa ni mmoja ya watu waliohuka kusimamia uuzwaji wa viwanja maeneo mengi.

“Viwanja Itega vilikuwa vinauzwa milioni tano, sasa vinauzwa milioni 25, hili hujalisikia wewe mtu wa CDA?” alimuhoji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa IST, Martin Chodota, aliomba Serikali kutoa kipaumbele kwa kampuni za wazawa na kuacha kuwapa nafasi zaidi wapimaji wanaotoka nje.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles