Na JUDITH NYANGE
SERIKALI imeombwa kutoa elimu ya namna ya kujiokoa kwa abiria wanaotumia usafiri wa majini kuepusha vifo vya watu wengi kama ilivyokuwa katika ajali ya meli ya MV Bukoba iliyotokea Mei 21, mwaka 1996.
Mmoja wa watu walionusurika katika ajali hiyo, Charles Limbu, alikuwa akizungumza wakati wa kumbukumbu ya miaka 21 tangu kutokea kwa ajali hiyo, zilizofanyika juzi katika makaburi ya Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza.
Alisema ni wakati sasa serikali kuhakisha elimu na vifaa vya kujiokoa vinakuwepo katika vyombo vyote vya usafiri wa majini.
“Abiria wengi hawafahamu namna ya kutumia maboya na vifaa vingine vya kujiokoa vilivyopo katika vyombo vya usafiri wa majini.
“Ni vema serikali ikahimiza na kuhakikisha wasafiri wanapatiwa elimu ya kutumia vifaa hivyo vya kujiokoa kupunguza madhara inapotokea ajali.
“Katika ajali ya MV Bukoba wengi tuliopona ni kwa sababu tuliweza kuzingatia elimu tuliyopatiwa wakati tunaanza safari.
“Nilipoona meli imeanza kupoteza uelekeo nilikimbia kuchukua boya ambalo lilinisaidia kujiokoa, laiti kama abiria wote wangekuwa wanafahamu namna ya kutumia vifaa hiyo kusingetokea vifo vya watu wengi,” alisema Limbu.
Limbu aliitaka serikali kuhakikisha vifaa hivyo vinakuwapo sehemu za wazi ambako abiria wote wanaweza kuvifikia na kwa idadi sawa kulingana na uwezo wa chombo husika.
Kiliphece Herman ambaye pia alinusurika katika ajali hiyo, alisema chanzo cha ajali hiyo ni umasikini wa kutumia kifaa chakavu kusafirishia abiria, ujinga wa jamii na viongozi wanaowajibika kusimamia usafiri na uzembe kwa wanaopewa jukumu la kuendesha na kusimamia vyombo hivyo.
“Bila mambo hayo kutatuliwa ajali za mara kwa mara zitaendelea kutikoea, nawashauri viongozi wa serikali kuichukua jukumu la kupunguza umaskini na kuhakikisha vinakuwapo vifaa bora vya usafiri.
“Kuondoa ujinga kwa walio na jukumu na mamlaka zinazohusika kusimamia vyombo vya usafiri hasa wa majini na kutoa adhabu kali kwa wale watakaobainika kufanya uzembe kwa kukiuka na kuvunja sheria zilizopo,” alisema Herman.
Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC), Eric Hamissi, aliwataka wananchi kuacha kuwa na hofu.
Aliwashauri wasione baada ya ajali hamna usalama wa usafiri wa majini kwa sababu baada ya tukio hilo zilichukuliwa hatua kubwa za kuhakikisha halijirudii na usalama wa abiria katika meli zao unazingatiwa kwa kiwango cha juu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema serikali ipo mbioni kununua meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri ndani ya Ziwa Victoria pamoja na kuzifanyia marekebisho na ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha usalama wa abiria wakati wote.
“Kila mtanzania kwa imani yake aendelea kuwaombea marehemu wote waliotangulia mbele ya haki na wote wenye jukumu na dhamana ya suala la usafirishaji.
“Kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake katika eneo lake ili kukomesha kabisa matukio ya ajali,” alisema Mongella.
Tukio hilo kubwa la historia la kuzama kwa meli ya MV Bukoba lilitokea alfajiri ya Mei 21, mwaka 1996 zikiwa zimebaki kilometa 56 kufika Bandari ya Mwanza.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 800 ambako watano kati yao walitambulika na familia zao na 130 waliweza kuokolewa.