Na JUDITH NYANGE
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Leonard Subi, kutoa muongozo wa jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa anapotokea mgojwa.
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoa tahadhari kuhusu kujikinga na mlipuko wa ugonjwa huo.
Hiyo ni baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kulipuka kwa ugonjwa huo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika jimbo la mpakani na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Tahadhari hiyo ilitolewa hasa katika mikoa ambayo inayopakana na DRC na mikoa iliyotakiwa tahadhari hiyo ni Mwanza, Kagera Kigoma, Katavi na Rukwa na Songwe.
Mongella alikuwa akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Alisema ni vema muongozo huo ukatolewa mapema ili anapotokea mgonjwa anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo taarifa zipatikane mapema na asiweze kuambukiza watu wengi.
“Mikoa iliyotajwa ambayo inaweza kuwa rahisi kupata ugonjwa wa ebola ni pamoja na Mwanza.
“Naomba utolewe mwongozo katika maeneo yote ya kuingia na kutoka Mkoa wa Mwanza pamoja na usafirishaji watu waweze kutambua na kama kuna dalili zozote za ugonjwa huo taarifa zitolewe mapema tusije tukachelewa ,” alisema Mongella.
Vilevile aliitaka bodi hiyo kuisimamia hospitali hiyo na kuhakikisha inaongeza mapato yake kutoka Sh bilioni moja zinazokusanywa sasa kwa mwaka hadi angalau Sh bilioni 2.5 au 3 kwa mwaka na kuhakikisha wanatumia mifumo ya eletroniki kudhibiti ubadhirifu.
“Tumeongeza makusanyo yetu kutoka Sh mlioni 500 hadi kufikia Sh bilioni 1 kwa mwaka.
“Lakini kwa idadi yetu ya watu tulipaswa kufikia Sh bilioni 2.5 hadi 3 kwa mwaka, bodi hii isimame imara kuhakikisha malengo hayo ya makusanyo yanafikiwa.
“Kuna tabia ya wizi wa dawa na vifaa vingine vya kutolea huduma na hili hakikisheni linakomeshwa.
“Haiwezekani kila siku watu wapewe maelekezo, gari linalotoka na kiasi kadhaa cha dawa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) lakini zinazofikishwa katika kituo husika si zote, niwatake watumishi wa afya waache ubadhilifu na wizi na kuwa waadilifu,” alisema Mongella.
Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Leonard Subi, alisema mahitaji halisi ya watumishi wa idara afya katika mkoa huo ni watumishi 7,582.
Alisema watumishi waliokuwapo kabla ya uhakiki walikuwa watumishi 3,552 ambao asilimia 48 ya mahitaji yote ya watumishi.
Dk. Subi alisema katika kukabiliana na tishio la mlipuko wa ebola wiki ijayo itaanza kutolewa elimu kwa wadau wote wa afya Mkoa wa Mwanza kuhusu ugonjwa huo.
Alisema pia itawekwa mikakati ya pamoja ya namna ya kuudhibiti na tahadhari za kuchukua endapo utatokea.