Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameunga mkono jitihada zinazofanywa na Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar za kusaidia wananchi wanaokabiliwa na hali duni ya maisha kwa kuahidi kutoa mifuko ya saruji 1,000 na mabati 600.
Samia, alitoa ahadi hiyo mjini Unguja jana, wakati anazindua kampeni maalumu ya ‘Mimi na Wewe’ inayolenga kuhamasisha wananchi kuungana pamoja kutoa misaada ya hali na mali ili kuboresha huduma za kijamii katika sekta za afya, elimu, mazingira, majisafi na salama, matumizi bora ya ardhi na kusaidia watu wasiojiweza.
Alikemea vikali tabia ya ubinafsi kwa baadhi ya viongozi, inayosababisha wananchi kutopatiwa taarifa muhimu za maendeleo yao hali inayosababisha uduni katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo.
Alisema ni muhimu kwa viongozi katika maeneo mbalimbali kujenga tabia ya kuweka wazi mapato na matumizi ya fedha wanazopata na jinsi zilivyotumika ili kuwapa moyo wananchi.
“Maendeleo endelevu ni lazima yazingatie utu na heshima ya mtu, mshikamano wa dhati na mafungamano ya kijamii,” alisema.
Pia alihimiza wadau mbalimbali wa maendeleo, hasa sekta binafsi na wananchi kujenga moyo wa kujitolea na kutoa misaada ili kuhakikisha taifa linasonga.
Alisema kampeni hiyo ina umuhimu wa kipekee, kwani inakusudia kuwaomba na kuwahamasisha wananchi, hasa wa Zanzibar kuchangia kwa hali na mali kusaidia wenzao ambao hali zao za maisha bado duni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud, alisema wameamua kuanzisha kampeni hiyo ili kurejesha moyo wa kusaidiana miongoni mwa Wazanzibar, hatua ambayo itasaidia maradufu uboreshaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Alisema mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wananchi wengi kwa Zanzibar, ambao ni zaidi ya 500,000.