Na Magreth Kinabo-Mahakama ya Tanzania
JAJI Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Ferdinand Wambali, amewataka Majaji na Mahakimu kuzingatia maadili ya uhakimu na utumishi wa umma.
Alisema hawana budi kutenda haki kwa wakati wanapokuwa kwenye majukumu yao.
Wambali amewataka majaji, mahakimu kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni za utendaji na za utumishi wa umma kama njia ya kukidhi mahitaji ya wananchi wanaowahudumia.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alipozungumza na baadhi ya majaji na mahakimu katika ofisi ndogo za Bunge.
“Suala la maadili lilianza tangu enzi za kale, jamii ilikuwa inajiwekea maadili, kuwapo maadili ni heshima na utii, tabia ya uaminifu, uwajibikaji na kufuata utaratibu kila unapotekeleza kazi,” alisema Jaji Wambali.
Alisema suala la maadili ni muhimu katika kupambana na rushwa kwa sababu linafanya jaji na hakimu awe na tabia njema mbele ya jamii.
Alisisitiza kuwa kazi hizo zinahitaji uadilifu na mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu.
Naye Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Beatrice Mutungi alisema lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili changamoto za kada hizo na kubadilishana uzoefu wakati wa kutatua changamoto hizo.