24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

DARASSA HESHIMA INAPANDA, INASHUKA!

NI shabiki gani wa kweli wa Bongo Fleva asiyemjua msanii Darassa? Ni mdau gani asiyeijua ngoma yake ya Muziki? Bila shaka wengi wanamuelewa vema huyu jamaa.

Darassa mwishoni mwa mwaka jana alionyesha kuwa msanii anayeweza asifurukete kwa mwaka mzima, lakini mwishoni akamaliza vizuri. Alidhihirisha kuwa muziki pamoja na mambo mengine ni kufanya tafiti na kucheza na akili za mashabiki.

Ngoma yake Muziki ilidhihirisha kuwa mwanamuziki anaweza akabadilika na kuwashika mashabiki wa rika zote kwa wakati mmoja. Darassa alifanikiwa pasi na shaka kuwaunganisha Watanzania.

Ngoma yake ikawa gumzo na kwa kweli ikawa kama wimbo wa Taifa, kutokana na kukubalika kwake na kupigwa kila mahali.

Ukienda baa unakutana nao, ukienda club habari ni Muziki na hata unapokuwa kwenye vyombo vya usafiri, wimbo uliopigwa zaidi ulikuwa ni Muziki.

Mpaka sasa Muziki bado unabamba sehemu mbalimbali za nchi yetu na hata nje ya nchi. Ngoma yenyewe inapagawisha zaidi kutokana na midundo yake na mashairi mazuri.

Kiukweli Darassa hajawahi kutoa ngoma ikaheat kwa kiasi kikubwa namna hiyo kama Muziki.Baada ya kimya cha muda mfupi, akiuacha wimbo huo uendelee kupeta mitaani, Darassa hivi karibuni ameachia ngoma nyingine.

Kibao hicho kinachokwenda kwa jina la Hasara Roho, kimeonekana kufanana kwa kiasi kikubwa sana na Muziki. Ingekuwa ameimba msanii msanii mwingine, tungesema bila kupepesa macho kuwa amemkopi Darassa kila kitu.

Lakini sasa kwa vile ni Darassa mwenyewe, hapa tunasema kuwa Darassa amekopi kazi yake mwenyewe na kupesti kwenye wimbo mwingine. Midundo na sauti, havina tofauti yoyote na Muziki.

Inawezekana kuna udhaifu sehemu kadhaa kwa Darassa na hasa utunzi wa mashairi na washauri wa awali – maana inapaswa kabla ya msanii kuachia ngoma yake ni vema awe na watu watakaosikiliza kwanza kabla ya kuachiwa.

Huenda hapakuwa na watu wa namna hiyo na kama walikuwepo walimshauri vibaya Darassa. Huko kwenye mitandao ya kijamii wadau wengi wametoa maoni yao wakieleza masikitiko yao kuhusiana na mfanano huo usio wa kawaida wa vibao vyake hivyo.

Vyovyote iwavyo, Hasara Roho hauwezi kufurukuta mbele ya Muziki ambao bado unaonekana kuwa bora mpaka sasa. Ushauri wangu wa mwisho kwa Darassa, akubali kushauriwa.

Ikiwa ana udhaifu wa kuandika mashairi, basi awape wenye uwezo huo wamsaidie. Kuteleza siyo kuanguka, Waswahili wamesema. Lakini pia kuanza upya siyo ujinga.

Bado Darassa ana nafasi ya kufanya ngoma nyingine kali itakayorudisha heshima iliyopunguzwa na Hasara Roho. Hakuna kinachoshindikana kwa Darassa maana kama ni sauti anayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles