NA SHOMARI BINDA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imekamata shehena ya sukari kutoka viwanda vya Kagera na Kilombero ikiwa inabadilishiwa kwenye mifuko ya Kiwanda cha Sukari cha Son Sugar cha i Kenya iweze kusafirishwa kwenda nchini humo.
Sukari hiyo ilikamatwa kwenye ghala la mfanyabiasha Maselo Ghati kwenye mpaka wa Sirari.
Mifuko 353 ya sukari kutoka kiwanda cha Kagera Sugar ilikamatwa ikihamishiwa kwenye mifuko ya kiwanda cha Son Sugar na kupelekwa Kenya.
Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Ernest Nkangaza, alisema operesheni inayoendeshwa na mamlaka hiyo kwa ushirikiano wa wananchi ndiko kulikofanikisha kukamatwa sukari hiyo.
Alisema katika tukio hilo, watu 20 walikamatwa pamoja na mmiliki ambao wanaendelea kuhojiwa na polisi sababu za kuibadilisha sukari ya Tanzania I ionekane inazalishwa Kenya wakati kukiwa na changamoto ya uhaba wa sukari na kupanda bei nchini.
Nkangaza alisema zipo hatua ambazo zitachukuliwa kwa mujibu wa baada ya taratibu mbalimbali kufuatwa.
Aliwataka wafanyabishara waache kufanya mambo kinyume na taratibu kwa kuwa mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti wote wasio waaminifu.
"Katika ghala la mfanyabiashara huyu tumekuta pia mifuko tupu ya Kiwanda cha Son Sugar cha Kenya pamoja na mifuko ya sukari ya Kagera Sugar na Kilombero, jambo ambalo linaonyesha kuna mchezo mchafu unaofanywa na mfanyabiashara huyu.
"Hili siyo jambo jema hasa ikizingatia kwa sasa kuna shida ya upatikanaji wa sukari na kupanda bei yake," alisema Nkangaza.
Ofisa Uhamiaji Mfawidhi Kituo cha Sirari, Estom Urio, amesema ni vema kukitumia vizuri kituo cha mpaka Sirari na kama mtu hajui ni vema aombe ushauri kwa kuwa hakuna gharama zozote kufanya biashara kwa uhuru.
Aliwashauri wafanyabiashara waache kufanya biashara zao kwa njia zisizofaa kwa kuwa kwa sasa maofisa wa serikali wanafanya kazi kwa kushirikiana hasa katika maeneo ya mipakani.