ABU DHABI, UAE
SHIRIKA la Anga la Etihad (EAG) limeanza mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya atakayetangazwa wiki chache zijazo baada ya aliyepo sasa kutarajia kustaafu.
Kama sehemu ya mchakato huo, Bodi ya Wakurugenzi ya EAG jana ilimteua, Ray Gammel kuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa shirika hilo kwa muda.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa sasa James Hogan atamaliza muda wake wa kulitumikia shirika hilo ifikapo Julai Mosi mwaka huu.
Ikiwa ni mipango ya mabadiliko ya kiuongozi, Gammel ataanza kutekeleza majukumu yake ya kiutawala kuanzia jana.
Gammel amekuwa na EAG tangu mwaka 2009 akishika nafasi ya Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu na Utendaji, ambapo alifanikiwa kuwaimarisha wafanyakazi kuwa na utendaji bora.
Pia alifanikiwa kujenga utamaduni wa uwajibikaji kazini kwa wafanyakazi pamoja na motisha, jambo ambalo limewawezesha kuongeza ukuaji wa kibiashara na kuinua Etihad kuwa miongoni mwa sehemu bora inayowavutia watu kufanya kazi duniani.