Na WAANDISHI WETU-DODOMA
BUNGE, jana lilipiga kura kuwachagua wabunge wawili wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema).
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya uliofanyika April 4 mwaka huu, kuahirishwa baada ya wagombea wawili wa chama hicho, Lawrance Masha na Ezekiah Wenje, kushindwa kupata kura za kutosha.
Wakati Masha na Wenje wakishindwa kupata kura za kutosha April 4, mwaka huu, wabunge wengine saba walichaguliwa wakiwamo sita kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Akitangaza uchaguzi huo jana, Katibu wa Bunge ambaye pia alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Dk. Thomas Kashilillah, aliwataja wagombea hao kuwa ni Profesa Abdallah Safari, Ezekiah Wenje, Josephine Lemoyang, Pamela Massay, Lawrance Masha na Salum Mwalimu.
Kwa mujibu wa Dk. Kashilillah, washindi wa uchaguzi huo wataungana na wenzao sita waliochaguliwa awali na kufanya idadi yao kuwa tisa ambayo ndiyo idadi ya wabunge wanaotakiwa kuiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki.
Aliyekuwa wa kwanza kuomba kura ni Profesa Safari ambaye aliwaomba wabunge wampe kura za kutosha akaiwakilishe nchi kwa kuwa ana uwezo na uzoefu wa kutosha katika masuala ya uongozi.
Pamoja na hayo, alisema ana uzoefu wa kutosha katika masuala ya siasa na kwamba amewahi kutunga vitabu sita ambavyo vinatumiwa katika vyuo na shule mbalimbali nchini.
Naye Wenje aliliambia Bunge, kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wa kuliwakilisha Taifa katika Bunge hilo kwa kuwa anaamini katika umoja na yuko tayari kupigania maslahi ya Taifa kupitia Bunge hilo.
Pia, alisema Hayati Mwalimu Nyerere alipoamua kuiingiza nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliamini katika umoja na mshikamano ambao hata yeye anauamini.
Kwa upande wake, Josephen alisema ana uzoefu katika masuala ya kutunga sera na masuala ya sheria kutokana na utumishi wake wa muda mrefu serikalini.
Naye Pamela alisema anastahili kuchaguliwa kwa kuwa ana uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya ubora wa bidhaa kwa kuwa ni mtumishi wa Kampuni ya kuzalisha vinywaji ya Coca Cola Kwanza.
Wakati hao wakisema hayo, Masha ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema anastahili kuchaguliwa kwa sababu ni mzalendo na kwamba alirudi kutoka Marekani na kurudi nchini kwa ajili ya kuja kulitumikia Taifa.
Pamoja na hayo, alisema kutokana na uzalendo uliotawala katika familia yao, mmoja wa ndugu zake ni mtumishi wa jeshi ingawa hakulitaja ni jeshi gani nchini.
Naye Salum Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), alisema anastahili kuchaguliwa kwa kuwa ana uwezo wa kulinda maslahi ya Taifa kupitia taaluma yake ya uandishi wa habari aliyoitumikia kwa muda mrefu katika moja ya chombo cha habari nchini.
Pia, alisema amewahi kufanya kazi kwa mafanikio katika Kampuni ya Simu Vodacom na kwamba ni mzalendo anayeweza kutetea maslahi ya Taifa.