VYETI FEKI VYAITESA SEKTA YA AFYA

0
1066

 

Na Waanidishi Wetu,

SUALA la uhakiki wa vyeti feki limezidi kuitikisa sekta ya afya ambapo maelfu ya watumishi wamejikuta wakipoteza kazi na zahanati na vituo vya afya vikifungwa.

Hatua hiyo inatokana na ripoti ya uhakiki wa watumishi wa umma nchini iliyokabidhiwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kwa Rais Dk. John Magufuli mjini Dodoma.

Katika sekeseke hilo watumishi 18 wa idara ya afya katika hospitali ya rufaa Bombo wamejikuta wakipoteza kazi kutokana na hali hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo,  Dk. Goodluck Mbwilo, alisema kuwa idara ya wauguzi ndiyo iliyoathirika zaidi.

“Eneo ambalo limeathirika zaidi ni idara ya uuguzi na kutokana na hilo wauguzi 13 wamebainika kuwa na vyeti feki, matabibu wawili na madereva watatu,” alisema Dk. Mbwilo

Kiteto

Watumishi 65 wamebainika kuwa na vyeti feki wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni sekta ya elimu na afya ambazo zinaongoza kwa watumishi wake kuathiriwa na hali hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Kambona, akizungumza na MTANZANIA amekiri kuathiriwa na zoezi hilo na kudai ongezeko la uhaba wa watumishi linazidi kukua.

Muleba

Uhakiki huo wa watumishio wenye vyeti vya kughushi umezidi kuathiri wananchi katika upatikanaji wa huduma za jamii katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wameondolewa  watumishi 53 kati yao 22  wanatoka idara ta afya.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Modest Lwakahemula, alisema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani    ambako alisema kwenye baadhi ya zahanati na vituo vya afya wananchi wanakosa huduma kutokana na hali hiyo.

Arusha

Watumishi  503 wa umma  wakiwamo wa idara ya afya na elimu, wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi.

Rungu hilo pia limemwangukia mwanasheria wa Halmashauri ya Arusha, DC, wakunga, walimu, madereva na wahudumu wa ofisi.

  Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega, aliiambia MTANZANIA jana kuwa  uhakiki huo ulifanywa kwa watumishi 15,777 huku sekta zilizoathiriwa zaidi ni afya, elimu na utawala.

Habari hii imeandaliwa na Amina Omari (Tanga), Abraham Gwandu (Arusha), MOHAMED HAMAD (Kiteto) na KAHINDE KAMUGISHA (Muleba).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here