24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAATHIRIKA WA AJALI WANAHAKI KULIPWA FIDIA

NA ALOYCE NDELEIO,

TANZANIA ipo katika simanzi kubwa baada ya kutokea ajali ya basi jijini Arusha ambayo ilisababisha  vifo vya wanafunzi 33, mwalimu wao pamoja na dereva wa basi hilo. Tukio hilo la kutisha ni mfululizo wa ajali ambazo zimekuwa zikitokea hapa nchini

Suala la ongezeko la ajali lilishajadiliwa bungeni  ambapo Juni 19, 2007 Mbunge wa Jimbo la Mlalo (wakati huo)  Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Athumani Ngwilizi (CCM ) aliuliza, “Kwa kuwa, ajali zinazosababishwa na vyombo vya usafiri wa barabarani, majini na njia ya anga zimekuwa zikisababisha vifo na majeruhi wengi na kwa kuwa, sheria zimeagiza kila chombo kinachojihusisha na biashara ya kusafirisha abiria kwa njia yoyote ile kiwe na bima ili wasafiri waweze kulipwa fidia pindi ajali zinapotokea:-

(a) Je, ni ajali ngapi za barabarani, majini na angani zimetokea katika kipindi cha mwaka 2005/2006 na ni abiria wangapi wamepoteza maisha na au kujeruhiwa, na kati ya hao ni abiria wangapi wamelipwa fidia kutokana na vyombo hivyo vya usafiri vilivyopata ajali hizo?

(b) Kwa kuwa, wananchi wengi wameathirika kutokana na ajali zinazosababishwa na vyombo hivyo vya usafiri, na wengi wao bado wanadai fidia wanazostahili huku wakiwa hawajui taratibu za kufuata ili kupata haki zote. Je, Serikali inatoa maelezo gani ili kuwasaidia wananchi hao kupata haki zao?  

Majibu yalikuwa, ”Wizara ya Miundombinu (kipindi hicho) ndiyo yenye dhamana ya kusimamia sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kuhakikisha kuwa usafirishaji wa abiria na mizigo unakuwa wa uhakika, salama na nafuu kwa pande zote zinazohusika. Katika kupambana na tatizo la ajali za barabarani, majini na angani wizara inashirikiana na Jeshi la Polisi na imeanzisha vyombo (3) vifuatavyo:- Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA); Kitengo cha Usalama Barabarani (RSU); na Wakala wa Usalama.

”Majukumu ya msingi ya vyombo hivi ni kuweka sera na mikakati ili kuhakikisha kuwa tatizo la usalama katika sekta ya usafiri na usafirishaji linadhibitiwa…

 ”Ni kweli kuwa baadhi ya wananchi wetu hawajui taratibu za kudai fidia na walio wengi hawana taarifa kuwa mtu anapopata ajali anastahili kulipwa fidia inayotokana na bima ya chombo alichosafiria.

Kwa majibu hayo ni kwamba Tanzania kunatokea ajali nyingi sana katika sekta ya usafirishaji, lakini waathirika wengi (majeruhi na wanaofariki) hawalipwi fidia yoyote.

Hivyo kampuni za bima zinapata faida kubwa kwa sababu, wahanga wengi wa ajali hawadai fidia za bima ingawa vyombo vya usafirishaji vinavyohusika katika ajali hizo vimekatiwa bima za lazima kisheria.

Kama wananchi wengi wangejua kuwa  wanatakiwa kulipwa fidia basi wangezisumbua kampuni za bima na kampuni hizo zingeshinikizwa kushiriki katika vita dhidi ya ajali za kizembe ili zisipoteze fedha nyingi kwa kulipa fidia waathirika.

Tunataarifiwa kwamba huko Marekani na Ulaya kampuni za bima zinaogopa sana kutoa bima kabla ya kutafiti historia ya mteja na kitu kinachokatiwa bima.

Hali ni tofauti hapa nchini, kwani inashangaza kuona kampuni za usafirishaji zenye magari yanayopata ajali mara kwa mara zikizidi kutajirika kutokana na malipo ya bima. Tena kila ajali kubwa inapotokea utasikia watu wakisema: ”Ah, mwenye gari hana hasara bwana… bima itamlipa gari mpya!”. Halikadhalika kampuni za bima hazitafiti kwa kina historia ya mteja kabla ya kupokea ombi la bima.

Kwa kuwa bado kampuni za bima na yenye vyombo vya usafirishaji zinapata faida licha ya ongezeko la ajali hapa nchini kuna haja ya kutafiti ili kupata suluhisho la ongezeko la ajali.

Katika nchi zilizoendelea kampuni za bima na vyombo vya usafirishaji huwa ndio wadhamini wa vipindi vya redio na televisheni vinavyotoa elimu kwa umma kuhusu tahadhari dhidi ya ajali. Hapa Tanzania hakuna kampuni ya bima au ya usafirishaji inayojisumbua kufanya hivyo kwa sababu zilizo wazi: Ajali zikiongezeka hazipunguzi faida ya kampuni hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles