22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

ASHA BALOZI: WANAOIVURUGA Z’BAR NI VIJANA WASIOJUA HISTORIA YA NCHI

Mke wa Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi

 

NA SARAH MOSSI

KATIKA sehemu ya kwanza ya Makala haya Mwandishi wetu SARAH MOSSI alifanya mahojiano na Mama Asha Balozi ambaye ni Mke wa Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Mama Asha ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wake za Viongozi Zanzibar na wanawake viongozi. Pamoja na kuwa mke wa kiongozi lakini ni mstaafu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na amefanya kazi kwa karibu sana takribani na marais waliopita wa Zanzibar akiwamo, Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi, Marehemu Idrissa Abdulwakil na Dk. Salmin Amour ” Komandoo”

Wengi wanaamini wanawake wanaweza kuwa ni ngumu kwao kuomba kura kwa niaba ya waume zao, lakini Asha ni miongoni mwa wanawake wachache waliojitokeza kumuombea kura mume wake, Balozi Seif Ali Iddi mwaka 2010 katika Jimbo la Kitope na hatimaye kuibuka kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Katika sehemu hii ya pili anaeleza nguvu ya wanawake katika uongozi…. Endelea.

MTANZANIA: Wewe ni mke wa kiongozi mkubwa Serikalini unawaeleza nini wanawake hususani katika kuwasaidia waume zao majimboni?

ASHA BALOZI: Asikwambie mtu wanawake wakikukubali utashinda tu, wanaume si watu wa kuaminika, asilimia kubwa ya kura zinatoka kwa wanawake ambao ndio wenye changamoto kwa sababu pakitokea tatizo la maji anayelia si mwanamume.

Changamoto yoyote katika familia ni ya mwanamke na ndiye mwenye mitihani na ndio wenye mzigo mkubwa wa kulea familia, kulea baba na watoto.

MTANZANIA: Unawezaje kumsaidia mume wako katika kuhamasisha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi katika kuleta maendeleo ya Zanzibar?

ASHA BALOZI: Hakuna mtu anayemkataa wake, lakini wanaoibomoa Zanzibar ni hao Diaspora…wanaoivuruga Zanzibar ni vijana wetu wanaoishi nje. Si kwamba Serikali haiwataki lakini hawana nia njema. Sasa hivi kafanye utafiti Pemba utagundua Pemba sasa inakwisha, maji ya chumvi yana kila kile kisiwa.

Angalieni Libya, walikuwa wakiishi vizuri lakini walioiingiza nchi katika matatizo ni wale Walibya wanaoishi nje ya nchi walioingizas siasa za nje.

Nchi zote unazoziona zinaingia katika mgogoro wa kivita ujue chanzo ni wale wananchi waliokuwa wakiishi nje ya nchi na kulishwa sumu.

Nchi za wenzetu hawana rasilimali kama tulizonazo sisi lakini watoto wetu hawataki kufikiri wanapenda kujivika siasa za nje na wala hajui wazee walitoka wapi na hii nchi ilikuwa vipi.

Na nikwambieni wenzetu hawataki kuona vyama vilivyopigania uhuru wa nchi vikiendelea kutawala. Juzi hapa walisema nchi ina njaa… ina njaa… Mimi nilikwenda hadi Katavi nilikuta chakula cha kutosha.

Ndio vile tunavyosema kuna watu wameona Magufuli kawabana. Maana hawa hata likizo walikuwa hawataki kwenda likizo na akiondoka kazini na milioni tano ndio wale wanaosema nchi ina njaa, hawa hawakuzoea kuishi kwa mishahara yao lakini mimi ninayegaiwa mshahara na mume wangu sioni njaa kwa sababu nimejua namna ya kuitumia bajeti yangu.

MTANZANIA: Wewe ni kati ya wanawake wachache waliobahatika kufanya kazi kwa karibu na viongozi wakuu wa SMZ, Je, vipi unazielezea siasa za Zanzibar zinavyokwenda kwa sasa?

ASHA BALOZI: Zanzibar ni shwari hakuna tatizo, watu wanakwenda kwenye sherehe za harusi hadi saa sita usiku, Je, nchi ambayo haikaliki utatembea hadi saa sita usiku? Wamesikia kuna tangazo la watu kutotembea ovyo?

Siku zote kitu kama hukipendi lazima ukitie dosari, lakini watalii wanakuja kama kawaida, ndege gani ilikuja ikachukua watu wake Zanzibar kwa sababu ya kukosekana usalama wa raia wao?

Utalii ndio unaotuendesha sisi sasa hivi na ndio maana utaona mishahara ya wafanyakazi wa Serikali imepanda kwa sababu ya mapato kuongezeka.

Tusiombe dua mbaya, kwani dua mbaya haombewi mtoto. Unapopata neema shukuru Mungu na ukikufuru Mwenyezi Mungu anakuleteeni mabaya. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Sisi hapa tukija kwenye uchaguzi ni tofauti na Bara, uchaguzi wetu unakuwa ni mgumu ni sawa na Mapinduzi.

MTANZANIA: Ulisema katika kusaidia vikundi vya kijamii ulisema hupendi kuingiza siasa, hili umefanikiwa vipi?

ASHA BALOZI: Hili napenda kulisimamia kwa nguvu zote na naona ninafanikiwa kwa asilimia kubwa, kwa sababu baadhi ya wakati ninaletewa misaada hususani wakati wa Mwezi wa Ramadhani, basi vijiji vyote vilivyo katika Jimbo la Kitope nimewaambia wote tupate futari kwa pamoja na fedha zao waziweke kwa ajili ya kuwatayarishia watoto sikukuu.

Kwahiyo ninachopata kama mchele, maharage, sukari na kila aina ya chakula tunakula kwa pamoja,

Hata kule Nungwi kuna vijiji vya Matemwe na Maweni hata ardhi yao ya kulima ni ngumu kwa kuota mazao, kwa hiyo Mwezi wa Ramadhani wote mimi napelekea chakula.

Wenyewe wanapika na mara moja moja nakwenda kupata futari nao kwa pamoja. Ninawapelekea chakula na pesa kila kikundi Sh milioni moja na hiyo ni kuanzia siku ya kwanza ya Mwezi wa Ramadhani hadi tunafungua.

Mimi sikujiingiza kwenye siasa na ndio maana utakuta hawaoni taabu kunisapoti. Ukijiingiza kwenye siasa utachukiwa na watu watakususa. Na misaada ninayotoa mpaka Pemba inakwenda

MTANZANIA: Nini kauli yako kwa wale wanaobeza Muungano?

ASHA BALOZI: Unapovunja Muungano ni hatari kwani hutoweza kumiliki ardhi Tanzania Bara, utakodishwa kama mgeni, Je, utasema umeonewa? Utasafiri kwa kutumia Pasipoti. Lakini siku zote wanasema “wagawe uwatawale”

MTANZANIA: Unafikiri uchumi wa Zanzibar unakua?

ASHA BALOZI: Uchumi wetu si mbaya, uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa pia na kama uchumi wetu usingekuwa unakua Rais, Dk. Shein asingeongeza mishahara kwa asilimia mia moja.

Unapoongeza mishahara maana yake ni kuwa uchumi wako ni mzuri, wakati fulani tuliwahi kukaa miezi mitatu hatutapata mishahara. Huko tunakokwenda akija mwingine naye ataongeza akipata.

Hasa walimu nasikia wamefurahi mishahara yao imepanda kweli kweli kwa sababu tangu awali mishahara yao ilikuwa ni mikubwa. Lazima tumshukuru Mwenyezi Mungu na kiongozi mwenyewe ameona kinachopatikana lazima wananchi nao wafurahi.

MTANZANIA: Unafanya kazi karibu sana na Mke wa Rais WA Zanzibar, Mama Manamwema, Je, una wito gani kwa kinamama?

ASHA BALOZI: Kwanza napenda kumshukuru mume wangu kwa kuniunga mkono kwa kila ninachopanga kukifanya katika kuwaletea kinamama, vijana na watoto wa Zanzibar maendeleo, namshukuru sana Mama Mwanamwema kwa kuwa nami bega kwa bega katika kazi zetu tunazozifanya kuwaletea maendeleo kinama wa Zanzibar.

Nawashukuru viongozi wote niliowahi kufanya kazi nao kwa karibu kwa kuniongoza hadi hapa nilipofika. Nawaombea dua kwa Mungu awape maisha memawazidi kufanikiwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles