32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MHESHIMIWA RAIS TUNA HAMU YA KUKUSIKIA

NA LEAH MWAINYEKULE,

TAIFA limepata msiba mkubwa.  Tangu kusikika kwa habari za ajali ya watoto, walimu pamoja na dereva wa shule ya Lucky Vicent iliyopo Arusha, kila mtu ameumia.  Itoshe tu kusema kwamba taifa limepoteza vijana wadogo ambao ndio viongozi wa kesho, madaktari wa kesho, walimu wa kesho, wafanyabiashara wa kesho, kinamama na kinababa wa kesho.  Inauma.

Kwa sisi kinamama, pindi tuliposikia taarifa za vifo hivyo, matumbo ya uzazi yaliuma.  Nina imani kwamba kwa kinababa pia, waliwawaza watoto wao ambao wapo shule na kujiuliza ingekuwaje endapo hilo lingetokea kwa uzao wao.  Kwa kinakaka, kinadada, wajomba, mashangazi, marafiki na hata majirani, kila mmoja wetu lazima alijiuliza maswali kadhaa na kupatwa na uchungu mkubwa.

Naomba niwape pole wafiwa wote.  Sitaki kuanza kufikiri wameumia kwa kiwango gani, lakini najua ni maumivu ambayo yanaweza yasifutike kamwe.  Pole pia kwetu Watanzania wote kwa kupoteza vijana hao 32 na walimu wao wawili na dereva wao mmoja.  Kama Taifa, lazima tuomboleze.

Ninapotamka kwamba kama Taifa lazima tuomboleze, ninamaanisha kila mmoja kwa nafasi yake.  Watoto kwa wakubwa, kinamama kwa kinababa, wanafunzi na raia wa kawaida, viongozi na wasio viongozi…na hasa, kiongozi wetu mkuu.

Ndiyo.  Hapa ninamzungumzia Rais wa nchi yetu, Dk. John Pombe Magufuli, ambaye ndiye Baba yetu  na ambaye sisi Watanzania tuna hamu kubwa ya kumsikia akizungumza  kwa sauti yake  kuelezea namna Taifa lilivyoumia kwa kuondokewa na watoto wale.

Mheshimiwa Rais, wewe ndiwe kiongozi mkuu wa nchi yetu.  Hiyo inamaanisha kwamba maadam umekubali kuchukua jukumu la kutuongoza, basi macho na masikio yetu yote yanakuwa kwako katika nyakati tofauti, tofauti: iwe nyakati za furaha, nyakati za huzuni, nyakati za heri na hata nyakati za hali ngumu.  Jambo likitokea, masikio yetu yote yanakuwa yametegwa kusikia Baba umejiandaa kutuambia nini.

Naomba niwe muwazi Mheshimiwa Rais.  Ajali ile ya watoto wa Shule ya Lucky Vicent ilipotokea, wote tuliamua, nina imani nawe pia uliumia.  Hata hivyo, nilikuwa nikisubiri kwa hamu niione sura yako ya pili,  sura ya majonzi, sauti ya masikitiko, ujumbe wa maombolezo.  Nilikuwa na hamu ya kumuona Baba akizungumza na wanawe, akiwaambia watulie kwa dakika moja kuwaombea watoto wale na hata akijikaza asitoe chozi!

Sikuwa natarajia kuona tu taarifa kwa vyombo vya habari kama ilivyozoeleka, kwani tukio lile si jambo lililozoeleka.  Sikuwa natarajia kusoma tu maandishi yanayosema Rais ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha… bali nilikuwa nasubiri ujumbe mkubwa kuliko huo, ujumbe wa Baba kwenda kwa wanawe, kuonyesha kwamba tuko pamoja katika maombolezo haya.

Sikuwa natarajia kuona ujumbe wa Twitter ukisambazwa, ukisema kwamba umepatwa na uchungu na majonzi makubwa ulipoona majeneza ya watoto na walezi wao waliopoteza maisha katika ajali ile ya basi.  Au ujumbe mwingine ukisema tumewapoteza mashujaa wetu katika elimu. Au ujumbe uliosema tunapoomboleza vifo vya wapendwa wetu tuendelee kuwa wamoja… Mheshimiwa Rais, hukuweza kuyasema hayo wewe mwenyewe, tukakuona na tukakusikia sisi watoto wako?

Ngoja nikuambie nilichokuwa natarajia.  Nilitarajia kuona na kusikia vipindi vya kawaida kwenye redio na televisheni vikikatishwa, watu wakisogelea redio zao na kutumbua macho mbele ya televisheni zao, huku kiongozi mkuu wa nchi, Mheshimiwa Rais mwenyewe, ukiwa na uso wenye huzuni na majonzi makubwa, ukizungumza nasi.  Maneno hayo hayo uliyoyaweka kwenye taarifa ya Ikulu, maneno hayo hayo uliyoyaweka kwenye tweets zako, maneno hayo hayo ambayo pengine umeyasema kwa wengine…nilitamani sana ningeyasikia kutoka kwako.  Niamini, lina uzito wa kipekee.

Ni pigo kubwa na inauma mno, kwa kundi la wanafunzi wa kutoka shule moja, kufariki kwa wakati mmoja, katika mazingira ambayo walifariki.  Tukiacha kabisa siasa pembeni, huu ulikuwa ndio wakati wa sisi kuiona sura yako ya pili,  ile ya ubaba kuondokewa na wanawe, ile sura ya huzuni, ile sura yenye uchungu mkubwa, ambayo ukiitazama, huwezi hata amini kwamba ni ya mtumbua majipu.

Mheshimiwa Rais, tuna hamu ya kukusikia.

[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles