PARIS, UFARANSA
RAIS Mteule wa Ufaransa, Emmanuel Macron, jana alianika mipango ya awali atakapoingia madarakani ikiwa ni pamoja na kuzuru Ujerumani na kubadilisha jina la vuguvugu lake la kisiasa.
Macron, ambaye anaunga mkono Umoja wa Ulaya (EU) alitangazwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais uliofanyika juzi baada ya kumshinda Kiongozi wa Chama chenye sera kali za mrengo wa kulia anayepinga wahamiaji na umoja huo, Marine Le Pen kwa asilimia 66 ya kura dhidi ya 33.
Akizungumza na wafuasi wake, Macron alisema, “Nitawatumikia kwa unyenyekevu kwa nguvu zote. Nitawatumikia kwa ari, uhuru, usawa na umoja. Nitawatumikia kwa uaminifu na kwa imani mliyonipa, nitawatumikia kwa mapenzi. Idumu jamhuri. Idumu Ufaransa!.
Macron, kwa sasa lazima atafute wingi wa viti katika uchaguzi wa Bunge utakaofanyika Juni mwaka huu kwa ajili ya vuguvugu lake la kisiasa lenye mwaka mmoja tangu kuundwa kwake.
Chama chake cha En Marche, kinachomaanisha ‘Kusonga Mbele’ kinabadilisha jina lake wakati kikiandaa majina ya wagombea ubunge.
Macron ameahidi nusu ya wagombea hao watakuwa wapya katika siasa za kuchaguliwa kama alivyokuwa yeye mwenyewe kabla ya uchaguzi huo wa urais.
Aidha Chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha National Front nacho kinajiandaa kubadilisha jina na kama si kurekebisha fikra zake baada ya kushindwa vibaya kwa Le Pen.
Katika mahojiano yaliyofanyika jana, Mkurugenzi wa Kampeni wa Le Pen, David Rachline, amesema chama hicho kilichoasisiwa na baba wa kiongozi huyo, kitapata jina jipya kama njia ya kuwavutia wapiga kura zaidi nchini Ufaransa.