Na Amina Omari,TANGA
JESHI la Polisi mkoani Tanga limemzuia Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro kufanya ziara ya siku mbili ya kukagua na kuimarisha shughuli za chama katika Wilaya ya Tanga kwa sababu za usalama.
Mtatiro alitakiwa kuanza ziara hiyo, Mei 6 hadi 7 na alilenga kufanya kikao cha kamati ya utendaji na shughuli za kuimarisha chama ikiwamo kufungua matawi na kupokea wanachama wapya.
Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Idi Abdallah, alisema walilazimika kusimamisha ziara hiyo baada ya kupokea taarifa za intelejensia zinazoonyesha kuwapo viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Tumepokea taarifa kutoka ndani ya chama kuwa ziara hiyo pamoja na mikutano isingeweza kuisha salama bila kuwapo matukio ya vurugu na umwagaji damu… kulinda amani ya wilaya yetu, tumeona tusimamishe ziara hii,”alisema Abdalla.
Kabla ya msafara wa Mtatiro kuwasili katika ofisi za CUF zilizoko Barabara ya 20, magari ya polisi yalikuwa yakifanya doria nje ya ofisi hiyo kwa ajili ya kulinda usalama.
Baada ya msafara wa kiongozi huyo kufika, uongozi wa wilaya uliombwa Kituo cha Polisi Chumbageni kwa ajili ya kuonana na OCD.
Viongozi wote walitii agizo hilo na kuwasili Chumbageni, ambako walikaa dakika 45 na baadaye kuruhusiwa kurudi kuzungumza na wanachama wao kuhusu maagizo waliyopewa.
Mtatiro aliwaeleza wanachama kuwa wamepewa agizo la kusimamisha shughuli zote ambazo zilikuwa zifanyike katika ziara hiyo kutokana na sababu za usalama.
Alisema wameamua kutii amri ya polisi kuepuka madhara ambayo yanaweza kuwapata wanachama wake.
“Sitaki mapambano ya wananchi na polisi yabakishe makovu na madhara, ninawaahidi nitakuja wakati mwingine hali itakapokuwa sawa kuendelea na majukumu ya kuimarisha chama,”alisema Mtatiro.
Hata hivyo, alitoa maagizo kwa madiwani wa chama hicho kumaliza tofauti zao na kuhakikisha wanaimarisha shughuli za chama ikiwamo kusimamia na kutetea ahadi walizotoa kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alisema msimamo wa wanachama katika wilaya hiyo ni kuwa hawaungi mkono vitendo vya uhujumu wa chama vinavyofanywa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba .
Mbunge wa Viti Maalum, Saumu Sakala (CUF), alionyesha kusikitishwa na kitendo cha polisi kuzuia mkutano huo.
Mwisho
Serikali: Tutaondoa vikwazo
biashara ya madini
Na Mwandishi Wetu, Arusha
WADAU wa madini wametakiwa kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini badala ya kusanifiwa nje ya nchi kuwezesha azma ya Tanzania ya viwanda kupitia sekta hiyo.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Madini Tanzania, Benjamin Mchampaka wakati wa kufunga maonyesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika Arusha.
Alisema uwapo wa shughuli za ukataji na unga'rishaji wa madini nchini, kutawezesha kuyaongezea thamani ikiwamo kupanua wigo wa ajira.
" Tanzania ya sasa ni ya viwanda, sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu vya kusanifu madini yetu. Kwanza tutayaongezea thamani, pili tutazalisha ajira kwa wingi," alisema Mchampaka.
Alisema Wizara ya Nishati na Madini, imewasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya biashara ya madini ili kuondoa kero ambazo ni kikwazo kwa Watanzania.
"Tunataka kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa madini wa Tanzania,tunapenda wafanyabiashara wetu washiriki kwa wingi katika maonesho haya. Ni fursa kubwa ya kibiashara kwao," alissema Mchwampaka.
Akizungumzia mnada wa madini ya Tanzanite uliofanyika juzi, alisema minada hiyo itaendelea kufanywa mara kwa mara kutokana na mchango wake katika sekta husika.
Katika mnada huo wa madini ya Tanzanite, kampuni 48 zilishiriki ambako madini ghafi ya Tanzanite kutoka Kampuni ya TanzaniteOne yenye gramu 691,060.33 ziliuzwa Dola za Marekani 3,161,860, ikiwa ni asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.
Katika maonyesho hayo, ujumbe wa Serikali ya Nigeria ulishiriki na kueleza kuwa ulikuja kujifunza.
Ujumbe wa Serikali ya Nigeria uliongozwa na Waziri wa Madini na Maendeleo ya Viwanda, Abubakar Bwari aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abbas Mohamed na ujumbe wa wafanyabiashara wa madini kutoka nchini humo.