30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI TANGA YAMPIGA ‘STOP’MTATIRO

Na Amina Omari,TANGA

JESHI la Polisi mkoani Tanga  limemzuia Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro kufanya ziara ya siku mbili ya kukagua na kuimarisha shughuli za chama katika Wilaya ya Tanga kwa sababu za usalama.

Mtatiro  alitakiwa kuanza ziara hiyo, Mei 6 hadi 7 na alilenga kufanya kikao cha kamati ya utendaji na shughuli za kuimarisha chama  ikiwamo kufungua matawi na kupokea wanachama wapya.

  Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Idi Abdallah, alisema walilazimika kusimamisha ziara hiyo  baada ya kupokea taarifa za intelejensia zinazoonyesha kuwapo  viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Tumepokea taarifa kutoka ndani ya chama kuwa ziara hiyo pamoja na mikutano  isingeweza kuisha salama bila  kuwapo matukio ya vurugu na umwagaji damu… kulinda amani ya wilaya yetu, tumeona tusimamishe ziara hii,”alisema Abdalla.

Kabla ya msafara wa Mtatiro kuwasili katika ofisi za CUF zilizoko Barabara ya 20, magari ya polisi yalikuwa yakifanya doria  nje ya ofisi hiyo kwa ajili ya kulinda usalama.

Baada ya msafara wa kiongozi huyo kufika, uongozi wa wilaya uliombwa Kituo cha Polisi Chumbageni kwa ajili ya kuonana na OCD.

Viongozi  wote walitii agizo hilo na kuwasili Chumbageni,  ambako walikaa dakika 45 na baadaye kuruhusiwa kurudi kuzungumza  na wanachama wao kuhusu maagizo waliyopewa.

Mtatiro aliwaeleza  wanachama   kuwa wamepewa agizo la kusimamisha shughuli zote ambazo zilikuwa zifanyike katika ziara hiyo kutokana na sababu za usalama.

Alisema wameamua kutii amri  ya polisi  kuepuka madhara ambayo yanaweza  kuwapata wanachama wake.

“Sitaki mapambano ya wananchi na polisi yabakishe makovu na madhara, ninawaahidi nitakuja wakati mwingine hali itakapokuwa sawa kuendelea na majukumu ya kuimarisha chama,”alisema Mtatiro.

Hata hivyo, alitoa maagizo kwa madiwani wa chama hicho kumaliza tofauti zao na kuhakikisha wanaimarisha  shughuli za chama  ikiwamo kusimamia na kutetea ahadi walizotoa kwa wananchi.

 Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alisema msimamo wa wanachama katika wilaya hiyo ni kuwa hawaungi mkono vitendo vya uhujumu wa chama vinavyofanywa na  Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba .

  Mbunge wa Viti Maalum, Saumu Sakala (CUF), alionyesha kusikitishwa na kitendo cha polisi kuzuia mkutano huo.

Mwisho

Serikali: Tutaondoa vikwazo

 biashara ya madini

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WADAU wa madini wametakiwa kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini badala ya kusanifiwa nje ya nchi   kuwezesha  azma ya  Tanzania ya viwanda kupitia  sekta  hiyo.

Hayo yalisemwa na Kamishna wa Madini Tanzania,   Benjamin Mchampaka wakati wa kufunga maonyesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika Arusha.

Alisema uwapo wa shughuli za ukataji na unga'rishaji wa madini nchini, kutawezesha kuyaongezea thamani ikiwamo kupanua wigo wa ajira.

" Tanzania ya sasa ni ya viwanda, sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu  vya kusanifu madini yetu. Kwanza tutayaongezea thamani, pili tutazalisha ajira kwa wingi," alisema Mchampaka.

Alisema Wizara ya Nishati na Madini, imewasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri  ya  biashara ya madini ili kuondoa kero  ambazo ni kikwazo  kwa Watanzania.

"Tunataka kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa madini wa Tanzania,tunapenda wafanyabiashara wetu washiriki kwa wingi katika maonesho haya. Ni fursa kubwa ya kibiashara kwao," alissema Mchwampaka.

Akizungumzia mnada wa madini ya Tanzanite uliofanyika juzi, alisema minada  hiyo  itaendelea kufanywa mara kwa mara kutokana na mchango wake katika sekta husika.

Katika mnada huo wa madini ya Tanzanite, kampuni 48 zilishiriki ambako madini ghafi ya  Tanzanite kutoka Kampuni ya TanzaniteOne  yenye gramu 691,060.33 ziliuzwa Dola za Marekani 3,161,860, ikiwa ni asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.

Katika maonyesho hayo, ujumbe wa Serikali ya Nigeria ulishiriki na kueleza kuwa ulikuja kujifunza.

Ujumbe wa Serikali ya Nigeria  uliongozwa na Waziri wa Madini  na  Maendeleo ya Viwanda, Abubakar Bwari aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abbas Mohamed na ujumbe wa wafanyabiashara wa madini kutoka nchini humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles