Na ATHUMANI MOHAMED
UNAPOFIKIRI kuhusu maisha jambo moja kubwa na la msingi kufahamu ni kwamba, hakuna mafanikio kwa njia ya mkato, kama yapo basi mkato wenyewe ni kuiba! Zaidi ya hapo ni juhudi, ubunifu na bidii katika shughuli zako za kila siku.
Ukiondoa hayo ni lazima uwe mtu mwenye mawazo mapya kila siku ya kukuingizia fedha. Ukikosa maono na mawazo mapya, utaendelea kuwa yuleyule kila siku.
Utabaki kuwa mtu wa visingizio vya hapa na pale kuhusu maisha yako, lakini ukweli ni kwamba utakuwa hujafikiri sawasawa kuhusu maisha.
Kanuni nyingine ya kawaida ambayo nimekuwa nikiieleza mara kwa mara ni ile ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato kwa wakati mmoja huku ukipunguza matumizi yako kwa kadiri unavyoweza.
Lakini katika somo hili naeleza namna ya kumtengeneza kijana kuja kuwa tajiri mkubwa na mwenye mafanikio kwenye maisha yake.
Hatuwezi kukwepa ukweli kuwa kila kitu lazima kiandaliwe. Hata utajiri unatayarishwa. Hauji tu ghafla. Ni suala la kutengeneza kwanza.
Ndiyo maana katika mada hii nawafundisha vijana njia bora za namna ya kujitengenezea utajiri baadaye.
Hakuna uchawi, ni kuyajua mambo ya msingi kuyafanya wakati wa ujana. Yanaweza kuwa yapo mambo mengi sana, lakini hapa nataja yale yenye umuhimu zaidi 20.
Tumeshaona mambo sita, sasa tunaendelea na nambari saba. Kwa hakika mambo haya, kama kijana akiyafuata kwa dhati na kuhakikisha anayatekeleza ni hakika kuwa utajiri utakuwa siyo jambo la kusikia au kuona kwa jamaa zake, bali yeye atakuwa miongoni mwa matajiri hao.
7. ASETI
Kijana anayejitambua lazima afikirie kuhusu aseti. Ni kweli unaweza kuwa na fedha kwa vile fedha ni kila kitu, lakini kuna wakati fedha hushuka thamani.
Aseti zinazoaminika zaidi ni mashamba, viwanja, nyumba na madini. Hivyo ni vitu ambavyo kamwe havishuki thamani na badala yake hupanda kila siku.
Jambo la kufurahisha ni kwamba, kununua kwa mfano kiwanja leo hii ni rahisi zaidi, maana baada ya miaka kumi, kiwanja hichohicho kinaweza kuwa kimepanda thamani kwa zaidi ya asilimia 100.
Kiwanja kilichonunuliwa kwa Tsh. 3 milioni leo hii, baada ya miaka mitano, kiwanja cha namna hiyo kinaweza kufikia hadi Tsh. 10 milioni au zaidi kulingana na namna eneo linavyopanda thamani.
Kwa kuwa wakati wa ujana inawezekana ukawa huna fedha nyingi sana, siyo lazima kununua kiwanja eneo la mjini. Unaweza kununua kiwanja chako hata nje kidogo ya mji na baada ya muda, thamani yake itakuwa juu zaidi.
Viwanja leo hii unaweza kununua kwa kulipa kwa awamu, ukifanya hivyo, baada ya miaka kadhaa unaweza kuwa na viwanja vingi, sehemu mbalimbali.
Utakuwa na uhuru wa kuamua hata kuuza viwanja viwili kwa bei nzuri kisha ukafanya ujenzi wa thamani ambao utakuongezea aseti zako.
Ikiwa una nafasi nzuri kifedha, madini kama dhahabu na almasi ni hazina nzuri pia. Ni jambo la kuangalia nafasi yako kifedha na jambo gani litangulie kabla ya jingine.
Kumbuka biashara siyo aseti kwani kuna wakati unaweza kufilisika. Hata hivyo kufungua biashara mbalimbali kutakuweka karibu zaidi na mafanikio maana utakuwa umetanua wigo wako wa kukuingizia fedha.
SHIKA DINI
Wanaokuwa karibu na Mungu, mafanikio kwao siyo jambo la kufikirika. Shika sana dini. Tafuta kumjua Mungu kwelikweli.
Kupitia imani yako, omba darasa maalumu la kupanua uelewa wako kuhusu Mungu. Mche Mungu kiukweli na hakikisha unasali/unaswali angalau kila asubuhi unapoamka, usiku kabla ya kulala na wakati wa chakula.
Ni jambo zuri pia kusali kabla ya kuanza kazi zako, safari za kikazi nk. Mambo ya kiroho ukiwa nayo karibu, mengine hujiongeza yenyewe na utashangaa namna unavyokuwa siku hadi siku.
Julikana kwenye nyumba za Ibada, shiriki kwenye Ibada, michango na kazi zinazohusu madhehebu yako kwa karibu.
Jambo la msingi zaidi, mbali na faida za kiroho na ulinzi wa Kimungu, itakuwa rahisi kwako kupata msaada pale utakapokuwa umepatwa na changamoto za kimaisha. Lakini pia siyo changamoto tu, unaweza kuwa na shughuli za kiroho, ukapata usaidizi mzuri kutokana na ukaribu wako na wenzako katika imani.
Somo letu litaendelea wiki ijayo.