23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DIAMOND, KIBA WASALITI WAKUBWA!

Na ALLY KAMWE

SALAAM Watanzania wenzangu. Ni matumaini yangu tu wazima wa roho na Mungu ameendelea kutupa imani ya kuishi tukipambana na changamoto mbili, tatu alizotuandikia.

Naam, sote tunaishi kulitimiza agano. Hakuna mjanja kati yetu anayeijua kesho wala mwenye kiburi cha kuirejesha jana, yatupasa kushukuru kwa kila pumzi tunayoitoa bila kujali tupo katika mazingira gani.

Tuseme ahsante Mungu kwa uhai, ni mapenzi yake yeye leo mimi naandika na wengine mtasoma, ahsante Mungu wetu.

Watanzania wenzangu. Enyi ndugu, jamaa na marafiki, ninaowafahamu na nisiowafahamu, naomba kwa dakika chache tu kila mmoja akumbuke thamani ya taifa letu.

Hebu tuikumbuke thamani ya bendera yetu, mipaka, utu na amani yetu tuliyonayo leo hii. Sisi Watanzania tuna sifa ya uungwana kwa sababu tunajua kupendana.

Tunajua kuthaminiana na kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe. Rafiki wa kwanza wa Mtanzania ni Mtanzania mwenzake!

Tunajua kushikamana licha ya tofauti ya kiitikadi tulizonazo, tunajua kupendana licha ya tofauti ya kiimani tulizonazo.

Kwa ajili ya Tanzania, tumefundishwa kulia na kucheka pamoja. Tanzania kwanza ndio kauli mbiu yetu. Binafsi nimeumizwa sana na kitendo kilichofanywa na vijana wetu wa Kitanzania, Diamond Platinumz na Ali Kiba.

Bila shaka majina yao si mageni kwenye bongo zetu, tunawafahamu sote. Wawili hawa ni wasanii wakubwa sana ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa miaka mingi sasa wamevuja jasho kuhakikisha ala ya muziki wa Tanzania inaheshimika ugenini. Kwa sauti zao, wameifanya sekta ya muziki ikue na kutoa mianya ya ajira kwa vijana wengine wa Kitanzania. Pongezi kwao!

Lakini labda wamesahau mchango wa Watanzania kwenye mafanikio yao wanayojivunia nayo leo hii kiasi cha kuanza kutudharau na kudharau taifa letu.

Ziko taarifa kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya uhamasishaji ya Serengeti Boys, Maulid Kitenge, kuwa Diamond na Ali Kiba wamegoma kutoa ushirikiano wa kuisaidia timu yetu ya Taifa ya Vijana (U-17).

Tukumbuke, Diamond na Kiba walipata heshima ya kuteuliwa na aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya michezo, Nape Nnauye ili watie nguvu yao ya kuhamasisha Watanzania waichangie Serengeti Boys ili iweze kufanya vyema kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17.

Sote tunafahamu hali ya wale vijana wetu ilivyo, licha ya jasho wanaondelea kuvuja kwa ajili ya ya taifa letu, bado wanahitaji mchango mkubwa kutoka kwetu.

TFF wamejikuna walipoweza na ndiyo maana wakaileta timu mikononi mwa Watanzania ili tuweze kupambana pamoja.

Sina hakika sana na kazi ya Diamond na Kiba ndani ya kamati ile, lakini naamini jukumu lao lilikuwa ni kutoa nyimbo ya pamoja kwa ajili ya kuhamasisha Watanzania waisapoti timu yetu ya vijana.

Muziki wao ungeweza kupenya zaidi kwenye mioyo ya Watanzania kuliko sauti za kina Kitenge na Charz Hilary. Kwanini hakuna nyimbo mpaka sasa?

Jibu rahisi ni kuwa Diamond na Kiba wamegoma kufanya hivyo. Kwanini wamegoma? Ukweli wanao wao kwenye nafsi zao.

Huenda ni maslahi, huenda ni ugomvi unaosemekana upo kati yao. Yote yanawezekana na yote ni upuuzi tu.

Kuna hasara gani kufanya kazi ya taifa? Tena kwa ajili ya wadogo zao? Ni ugomvi gani huo waliokuwa nao hadi wakalisusa taifa namna hii?

Wametukosea sana, ni wasaliti. Tuliwapokea kwa mikono yetu, tukawalea, tukawathamini na kuwapenda. Tukawapa imani zetu na wakafanikiwa.

Lol! Leo wamesahau kila kitu? Wameiacha Serengeti Boys yatima? Kweli ‘Jeuri ya mjinga ndiyo upumbavu wake’.

Kwa sasa hatuna uwezo wa kuwapokonya walichochuma kutoka kwetu, acha wabaki na viburi vyao, sisi tuwapuuze tu.

Tusinunue wala kusikiliza tena nyimbo zao, mapromota wasiandae shoo yoyote ndani ya ardhi hii inayowahusu wao, tuwaache waendee na shoo zao za nje, sisi tuwapuuze tu.

Tuwapuuze kwa usaliti wao, tuwachukie kwa ujinga wao. Tuwapige vita kwa kiburi chao na dharau zao za kutoithamini bendera yetu takatifu.

Nitashangaa sana nikisikia wameitwa Ikulu au majina yao  yakizungumzwa ndani ya Bunge letu tukufu, ikiwa wameweza kudharau wito wa wizara, wataheshimu lipi tena la Tanzania?

Diamond na Kiba hawajaigomea kamati peke yake, bali wametugomea Watanzania wote. Diamond na Kiba hawajaisusa Serengeti Boys pekee, ila wameisusa na kuipuuza nia njema ya Rais John Magufuli, kuona sekta ya michezo ikizidi kukua na kuongeza fursa ya ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Asiye rafiki na Tanzania yetu ni adui yetu, tusiwachekee. Tanzania kwanza, Serengeti Boys ni yetu sote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles