28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

TENGENEZENI KIKI KWA NAMNA TOFAUTI

BAADHI ya wasanii wa Bongo wanaumwa ugonjwa wa kiki. Kila kukicha wanawaza mbinu za kutengeneza skendo yoyote kwenye mitandao ya kijamii na magazetini ili wapate kiki na wazidi kuwa juu kisanii.

Kiki ni ugonjwa mbaya sana na kwa bahati mbaya, kila msanii anaamini ataweza kufanya vizuri kupitia kiki. Kama Diamond ameweza kuwa juu kwa sababu ya kutengeneza skendo na kuzifanya kama daraja la mafanikio yake kimuziki, hiyo ni staili na bahati yake.

Hebu tumwangalie msanii mkongwe kama Jaydee. Ni lini Jaydee amekuwa na skendo? Lakini je, amewahi kushuka kimuziki mpaka sasa? Jaydee siku zote haandikwi kwa skendo bali habari ambazo zinatokana na kinachoendelea katika maisha yake.

Lakini wasanii wetu wa siku hizi wameibuka na ukichaa wa kusaka skendo kwa hali yoyote. Ya kazi gani basi? Waulize AY, FA, Sugu, Profesa Jay, ni lini walitegemea skendo kama mtaji wao kisanii?

Ok! Basi sawa… tuachane na hayo. Ipo dawa ya huo ugonjwa. Pamoja na mambo mengine, naamini kufanya kolabo na wasanii wengine wa ndani na nje ya nchi kunaweza kumpandisha msanii zaidi.

Wasanii wa enzi na enzi walitumia mbinu hiyo. Sikiliza kibao cha I’m Your Angel cha Celine Dion na R – Kelly unaweza kuelewa ninachomaanisha.

Rudi tena kwa Mfalme wa Pop duniani, marehemu Michael Jackson kwenye Love Never Felt So Good akiwa amemshirikisha Justin Timberlake… unaelewa lakini?

Hapa Bongo naamini kati ya wasanii waliofanya kolabo na wasanii wengi zaidi ni pamoja na Jaydee, Juma Nature, Dully Sykes, Chid Benz, marehemu Mangwair na Ali Kiba. Hawa hawajali, hata kama ni underground wapo tayari kushirikishwa.

Wengine wamefanya kolabo za kimataifa na kuwapaisha zaidi. Mifano ipo. Kuna Usiende Mbali (Bushoke na Juliana), My Number One Remix (Diamond na Davido) na  Kidogo (Diamond na P – Spuare). Orodha inaendelea.

Bila kupepesa ni kwamba Diamond anazidi kupata mafanikio kwa sasa kwa sababu anafanya kolabo nyingi zaidi za kimataifa; na hii siyo kwenye muziki tu, hata filamu.

Marehemu Steven Kanumba aliona mbali kwenye hilo. Kwa muda mfupi wa maisha yake kisanii, alifanya kolabo na wasanii wengi wakubwa wa Afrika. Mpaka sasa hakuna aliyevunja rekodi yake.

Bado mnang’ang’ania kiki za skendo? Mnaachwa na muda.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles