Na FERDNANDA MBAMILA
-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Watumishi Housing (WHC) imekabidhi nyumba sita za walimu wa Shule ya Sekondari Duga, iliyopo Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, lengo ni kuwasaidia kukabiliana na changamoto ya mazingira magumu ya kufanyia kazi inayowakabili walimu nchini.
Akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni, wakati wa makabidhiano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa WHC, Mhandisi Lwitiko Mndobo, ambaye ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi, alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapata nyumba bora ili waweze kufanya kazi zao ipasavyo.
“Kama watekelezaji wa mradi huu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu (TEA), lengo ni kuhakikisha kuwa tunajenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi wa umma na ndicho ambacho tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha kuwa tunasaidia serikali kupunguza nyumba za bei nafuu.
“Tunatambua kuwa mahitaji ya nyumba za watumishi ni makubwa, hivyo wito wetu ni kupata ushirikiano kwa mamlaka za wilaya zinazohusika ili tuweze kujenga nyumba bora kwa watumishi kulingana na mahitaji na thamani ya fedha,” alisema Mhandisi Mndobo.
Akipokea nyumba hizo kwa niaba ya Mkurugenzi, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mkinga, Omary Kombo, alisema nyumba hizo zitawasaidia walimu kuondokana na adha ya kuishi mbali na shule.
“Tumepokea vyema nyumba hizi, tunaamini kukamilika kwake zitakuwa na uwezo wa kuchukua walimu sita na hivyo itaondoa adha za walimu wetu wanaopanga mitaani na kusaidia kuongeza hadhi ya juu kwa walimu.
“Ni wazi kuwa serikali yetu sasa hivi inawathamini walimu wake, kwani hakuna aliyetegemea kuwa tungepata nyumba hizi katika miaka ya hivi karibuni, pia ni nyumba ambazo zimechukua muda, ikilinganishwa na nyingine zinazojengwa na wakandarasi wa ndani, hivyo tunawashukuru WHC na TEA na sisi tumezipokea na tutazilinda,” alisema Kombo.
Upande wake, ofisa rasilimali watu kutoka TEA, Richard Chiteji, alisema kwa sasa wanatekeleza miradi mbalimbali kwenye wilaya 40 ambapo kila shule itakuwa na nyumba moja yenye uwezo wa kupokea walimu sita, huku akiwataka wanufaika wa mradi huo kuzitunza nyumba hizo ili kuwa mfano kwa taasisi nyingine kupitia mradi huo.